Hatua mpya kukabili maambukizi ya VVU vyuoni

MOROGORO: SERIKALI inaendelea kuweka jitihada kubwa katika kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa kununua na kufunga mashine za kutolea huduma za kinga na Kipimo vitepe vya JIPIME kupitia mashine ya Ugavi wa Kidijitali kwenye vyuo vya elimu juu .
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu ,Profesa Paramagamba Kabudi amesema hayo wakati wa ziara yake mkoani Morogoro kuangalia Miradi inayotekelezwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Profesa Kabudi amesema Serikali itaendelea kutumia rasirimali zake za ndani kuendeleza miradi au program za Ukimwi na mingine baada ya wahisani kupunguza ufadhili hasa kwenye sekta ya afya pamoja na kuwepo mashirikiano na Mashirika ya Kimataifa.
“ Uhisani unapungua dunia nzima na vipaumbele vinabadilika na wao wanaamini baada ya miaka mingi ya uhisani wanaona nchi husika zitakuwa zimeanza kujitegemea,“ amesema Profesa Kabudi.

Profesa Kabudi amesema katika kuzuia maambukizi mapya ya VVU, Serikali imeweka jitihada kubwa kwenye uwekezaji wa viwanda vya kutengeneza dawa, chanjo na vifaa tiba.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imekuja na mipango na imetoa uwekezaji mkubwa ili kuifanya TACAIDS na program zote za VVU ziweze kuwa endelevu na mipango hiyo izidi kuendelea.
Profesa Kabudi amesema katika kipindi hiki, Serikali imeanza kujimarisha kwa kuwekeza katika ujenzi wa viwanda ili ifikapo mwaka 2030 Taifa liweze kujitegemea kwenye dawa, vifaa tiba na chanjo kwa asilimia 60.
Pia Serikali itaendelea kuhimiza utoaji wa elimu kwa jamii wakiwemo vijana ili waweze kupima afya zao na kuanza tiba mapema kwa wale watakaoonekana kupata maambukizi ya VVU.
“ Ili kupunguza maambuziki mapya ya VVU ni budi kuendeleza afua ya kuongeza kasi ya utoaji wa elimu hasa kwenye rika zinaloathirika zaidi, kuwapa nyenzo na vifaa vya kinga na kwa wale ambao wameathirika kuwahakikishia upatikanaji wa d awa na huduma,”amesema Profesa Kabudi.

Pia ametoa wito kwa klabu ya Afya ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na vyuo vingine kuendelea kutoa elimu kuhusu maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk Adam Mrisho amesema jumla ya mashine kumi zimefungwa kwenye vyuo sita vya elimu ya juu zenye thamani ya Sh : Milioni 168.
Dk Mrisho amesema Mashine hizo zinazojulikana kama Digital Vending Machine zimekua zikitoa huduma ya kondomu za kiume na za kike pamoja na Vitepe vya JIPIME.
Amesema mkakati Serikali ni kuhakikisha mpaka ifikapo Desemba mwaka huu (2026) mashine 65 ziwe zimefungwa kwenye maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu vikiwemo vituo vya mabasi, SGR, migodini, mwaroni na maeneo mengine.
Awali mtaalamu wa ufungaji mashine hizo, Dk Bonus Caesar ametaja vyuo vilivyofungiwa machine ni Chuo Kikuu SUA, Mzumbe, UDOM, Chuo cha Mipango, Chuo cha CBE na Chuo cha Hombolo.
“Mashine hizi licha ya kutoa kondomu za kike na za kiume pia zinatoa kipimo cha Vitepe vya JIPIME kwa kutumia mate, hii imesaidia kuwa na usiri wa taarifa pia kusogeza huduma za upimaji,” amesema Caesar.



