Kubecha afanya ziara, atatua mgogoro kijiji cha Lukando

GAIRO: Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Japhari Kubecha amefanya ziara katika Kata ya Chanjale, Kijiji cha Lukando, kwa lengo la kusikiliza wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili.
Katika ziara hiyo, aliambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.

Moja ya mafanikio makubwa ya ziara hiyo ni kutatuliwa kwa mgogoro wa muda mrefu uliokuwa kati ya Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kijiji cha Lukando, ambao ulikuwa umesababisha kukwamisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Baada ya kikao kilichowakutanisha viongozi na wananchi, Mwenyekiti wa Kijiji aliomba msamaha.
Wananchi walikubali ombi hilo na kuridhia aendelee kuiongoza kijiji, huku wakiahidi kushirikiana kuhakikisha maendeleo yanaendelea kwa manufaa ya wakazi wote wa Lukando.



