CUF: Misingi ya Waasisi Ilindwe

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimewataka Watanzania kuendelea kujifunza kutoka kwa waasisi wa taifa katika kulinda amani, umoja na mshikamano, kikisema misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, bado ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi.

Akizungumza na Daily News Digital, Mkurugenzi wa Siasa na Masuala ya Umma wa CUF Zanzibar, Ali Makame Issa, amesema Mwalimu Nyerere aliweka msingi wa taifa lenye umoja uliovuka tofauti za kisiasa, kiitikadi, kikabila, kidini na kikanda, jambo linalopaswa kuendelea kuwa dira kwa viongozi na wananchi.

Amewataka Watanzania kuendeleza utamaduni wa mazungumzo na uvumilivu wa kisiasa, akisisitiza kuwa amani ya kudumu inaweza kupatikana pale ambapo maslahi ya taifa yatawekwa mbele kuliko maslahi ya kisiasa ya vyama. “Tunaamini yanayotokea Zanzibar sasa yatatoa funzo muhimu kwa Watanzania wote kwamba licha ya tofauti zetu za kisiasa, sisi ni taifa moja lenye wajibu wa kulinda umoja, amani na Muungano wetu,” alisema.

Amesema maridhiano hayo yanaakisi kiu ya muda mrefu ya Wazanzibari ya kuishi kwa amani na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau wa kisiasa, hususan baada ya vipindi vya uchaguzi vilivyoambatana na mvutano wa kisiasa. SOMA: Nchome asisitiza kulinda amani

Aidha, alisema juhudi za mazungumzo zinazoongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kushirikiana na viongozi wa kisiasa, zimerejesha matumaini ya kujenga Zanzibar yenye umoja, maelewano na ushirikiano. “Hatua hii inatoa fursa ya kujenga umoja wa kweli na maridhiano ya kudumu. Kwa miaka mingi tofauti za kisiasa zimeleta mgawanyiko, lakini juhudi hizi zinaweza kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kwa manufaa ya Wazanzibari wote,” alisema.

Ameongezea kuwa mafanikio ya maridhiano hayo yataimarisha utulivu wa kisiasa na kuweka mazingira bora ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuwa viongozi na wananchi wataelekeza nguvu katika maendeleo badala ya migogoro ya kisiasa. Makame amesema amani na utulivu wa Zanzibar ni sehemu muhimu ya kudumisha amani ya Tanzania kwa ujumla, akisisitiza kuwa umoja wa kitaifa umeendelea kuwa nguzo ya mafanikio ya nchi tangu ilipopata uhuru.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button