TEWW yawarejesha wasichana masomoni

KATIKA kuhakikisha kuwa wanafunzi hao wanarudi shule kuendelea na masomo, serikali kupitia Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Ofisi ya Rais – TAMISEMI)  walianzisha mradi wa kuwasaidia wasichana waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali kupata elimu bure.

Mradi huo ulianzishwa kupitia Taasisi ya Elimu wa Watu Wazima (TEWW)  na kuitwa Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala. Kwa mujibu wa Mratibu wa mradi  huo ,Baraka Kionywaki anasema          mradi huo ulioanza mwaka 2022 ulilenga kuwarejesha wasichana 12,000 waliokatisha masomo kutokana na ujauzito na sababu nyingine.

Hata hivyo, hadi sasa wasichana 15,334 tayari wamerudishwa shuleni, idadi iliyovuka lengo la awali na Wizara ya Elimu, TAMISEMI na Benki ya Dunia.Kionywaki anasema awali kulikuwa na vituo 150 vya elimu ya sekondari kwa njia mbadala, lakini sasa vimeongezeka na kufikia 191 nchini kote ili kuwafikia wasichana wengi zaidi.

Anasema mbali na masomo ya kawaida, wanafunzi hupata mafunzo ya stadi za maisha, ujasiriamali, matumizi ya TEHAMA na ushauri wa kisaikolojia ili kuwasaidia kujenga upya maisha yao. Anasema mwaka huu pekee wanafunzi 401 wamefanikiwa kuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano au vyuo vya kati, ishara kuwa mpango huo umeanza kuzaa matunda.

Kionywaki anasema katika vituo 14 vya mfano tayari kumeanzishwa sehemu za kulelea watoto, mabweni ya mama na mtoto pamoja na wahudumu wanaowatunza watoto wakati mama zao wakiwa madarasani. “Kituo cha Vijaliwa Vingi kilichopo Mlandizi Mkoani Pwani ni miongoni mwa vituo hivyo,”anasisitiza.

Waziri  wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda, anasema Serikali itaendelea kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa haki ya kupata elimu, ikiwemo mabinti waliopata ujauzito, kama sehemu ya juhudi za kuimarisha usawa na ujumuishi katika sekta ya elimu nchini.

Prof Mkenda anasema kuwa  serikali imeendelea kuiweka elimu miongoni mwa vipaumbele vyake vya maendeleo, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga jamii yenye maarifa na ujuzi. “Rais Samia Suluhu Hassan anasisitiza kuwa kila mtoto wa Kitanzania lazima apate elimu. Kwa msingi huo, Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha usawa na ujumuishi katika elimu kwa watoto wote,” anasema Prof Mkenda.

Anasisitiza,“Hakuna mtoto atakayeachwa nyuma katika mfumo wa elimu. Hata mabinti waliopata ujauzito wanaruhusiwa na wanapaswa kurejea shuleni kuendelea na masomo yao. Anasema wanaendelea kuboresha mazingira ya shule ili yawe salama na rafiki kwa watoto wote.

Kwa upande wake, Katibu wa Mtandao wa Wazee wa Mila Tanzania, Chifu Girihuida Gegasa Shulumbu, anasema jamii ina wajibu wa kubadili mtazamo wake na kuwasaidia wasichana walipata mimba shule badala ya kuwasema vibaya. Anasema badala ya kuwanyanyapaa wasichana waliopata ujauzito, jamii inapaswa kuwaunga mkono kwa sababu wengi wao bado wana uwezo wa kuwa wataalamu na viongozi wa kesho.

“Tumeshuhudia wanawake waliowahi kupitia changamoto hizo wakawa madaktari, walimu, manesi, wahandisi na viongozi.,” anasema. Mtazamo huo unaungwa mkono na mdau wa elimu kutoka HakiElimu, Florige Lyelu, anayesema sera ya kuwaruhusu wasichana kurejea shuleni imefungua ukurasa mpya wa haki ya elimu nchini.

Hata hivyo anashauri serikali na wadau kuongeza vituo vya kulelea watoto, huduma za ushauri nasaha na ufadhili wa mahitaji mengine ya elimu ili kuhakikisha wanaorejea shuleni hawakatishi tena masomo yao. SOMA: Simulizi machungu kuozeshwa utotoni

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button