Simulizi machungu kuozeshwa utotoni

ILIKUWA safari ya takribani saa 24 kutoka Dar es Salaam hadi Kijiji cha Chasalawi kilichopo Kata ya Bupamwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza. Kijiji hiki kimepakana na Vijiji vya Mhalo na Sangu.
Safari hii ililenga kubaini vitendo vya ukatili dhidi ya wasichana ambao wanaolewa chini ya umri wa miaka 18.
Wenyeji wa eneo hili ni jamii ya Wasukuma, ambao wanadhani kwamba suala la mtoto wa kike kuolewa chini ya umri huo ni sahihi huku ikimfanya kama kitega uchumi na sababu ya kuondokana na umasikini wa familia kwa kupokea ng’ombe kama mahari, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, kijiji hiki cha Chasalawi kina wakazi wapatao 4,627 huku kaya 104 zipo chini ya Mpango wa Kunusuru Kaya masikini (TASAF).
Shughuli kuu za uzalishaji zinazofanywa na wakazi wa kijiji hiki ni kilimo na ufugaji. Wenyeji wanaeleza kwamba wanalima mazao ya mpunga, dengu, choroko, mahindi na njugu mawe ambayo hutumika kama chakula na kuuza kwa ajili ya kupata mahitaji mengine ya nyumbani.
Ardhi yake ni yenye udongo mwekundi na mweusi na nyumba za wanakijiji hawa zimejengwa kwa kutumia matofali ya tope (si ya kuchoma wala ya saruji) na zimeezekwa kwa bati.
Huduma za kijamii zinazopatikana kijijini hapa ni umeme kwa baadhi ya kaya zilizopo maeneo ya barabarani, shule ya msingi na maji ambayo hupatikana kwa Sh. 100 kwa ndoo tatu.
Wananchi wengine hutumia tochi au taa zinazotumia nishati ya umeme jua (solar) kwa ajili ya kuangazia wakati wa usiku.
Hata hivyo, shule ya sekondari ya kata wanayotumia watoto hao ipo umbali wa takribani kilometa 10. Umbali huu umekuwa kikwazo kwa baadhi ya wanafunzi kuhuduria masomo ipasavyo. Kutokana na hali hiyo wanashawishiwa na kukatishwa tamaa na wazazi na wanakijiji wengine, hivyo kusababisha watoto wengine kuacha shule na kuingia katika makundi rika ikiwemo makundi ya vijana wanaojihusisha na kilimo maarufu luganda.
Kadhalika, hakuna zahanati hivyo wanakijiji hao hulazimika kwenda Kituo cha Afya cha Mwamashimba umbali wa takribani kilometa 20.
Mtindo wa maisha wa familia hizi, huishi pamoja kuanzia baba mwenye kaya, watoto hadi wajukuu, hivyo kuna nyumba zenye vyumba viwili au kimoja na sebule zaidi ya mbili katika eneo moja la familia.
Hii huwafanya kukusanyika pamoja wakati wa kula na hata kusaidiana wakati wa kulima na kuvuna mazao, huku wajukuu wakihusishwa katika kuchunga mifugo ikiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Kwa mantiki hiyo, familia hizi ni masikini licha ya kuwa na mifugo ambayo kwao hutumia kulimia na mingine ni kama mapambo au fahari.
Ndoa za utotoni
Lengo la kutembelea kijiji hapa ni kutaka kujua undani wa ndoa za utotoni katika eneo hili. Wakazi wa eneo hili wanakiri kwamba vitendo hivyo bado vipo na kuhoji umri sahihi wa mtoto wa kike kuolewa.
Kauli hiyo inaungwa mkono na matokeo ya takwimu za jinsia inayojulikana kama Social Institution and Gender Index (SIGI) ya mwaka 2022, inayoonesha asilimia 19 ya wanawake wenye miaka 15 waliolewa kabla ya kufikisha miaka 18 na asilimia 16 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 24, waliolewa kabla ya umri wa miaka 18.
Hayo ni matokeo ya mila na desturi potofu pamoja na Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ambayo kwayo inakwenda kinyume cha Sheria ya Mtoto yam waka 2009; Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (ingawa haijataja umri wa mtoto, ile tu kueleza umri wa kuweza kupiga kura ni miaka 18, inamaanisha ndiyo umri wa mtu kuwa na haki ya kujiamulia mambo yake binafsi bila uangalizi); pia mikataba mbalimbali ya haki za binadamu iliyosainiwa na serikali.
Vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya ndoa, vinatamka kwamba mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 au 15 anaweza kuolewa kwa kibali cha mzazi, huku ikimnyima haki ya msingi ya kupata elimu na kuchangia athari za kiafya ikiwemo vifo vya uzazi kutokana na viungo vyao kutokuwa tayari kubeba majukumu hayo na athari nyingine za kijamii na kiuchumi.
Miongoni mwa waathirika wa ndoa za utotoni ni mama wa watoto wanne mwenye umri wa miaka 25 (hakutaka jina lake kuandikwa) anasema aliolewa akiwa na miaka 15 baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na kukosa ada.
Sasa ni miaka 10 ya kuishi katika ndoa ambayo hata hivyo, haitambuliki kanisani. Anakiri kwamba ndoa katika umri mdogo aliyoolewa, anapitia mateso, matusi na vipigo kutoka kwa mumewe.
Anasema aliolewa mwaka 2016 na moja kwa moja alifikia ukweni ambako alikuta familia yenye watu zaidi ya 20 wa rika tofauti na kwa kuwa alikuwa mke wa mtoto mkubwa wa mwenye kaya, alilazimika kufanya shughuli zote za nyumbani bila kupumzika.
“Nakumbuka siku moja nilishika vibaya maksai (ng’ombe za kulimia), mume wangu alinipiga sana na nguvu ya kurudi nyumbani kwetu sikuwa nayo kwa sababu baba alipokea mahari ya ng’ombe, na nikirudi kwetu ina maana baba atapaswa kuzirudisha,” anasema.
Anaongeza kuwa: “Nilikuwa napika chakula cha familia nzima, nachota maji ndoo hata nane kwa kufata ramboni wa umbali wa mita 200 na kwamba alihitajika kuosha vyombo, kiukweli kazi zilikuwa zikinielemea hadi wakati mwingine nilikuwa nalia.”
Anasema alishika ujauzito wa kwanza akiwa na miezi minne ya ndoa, lakini iliharibika ikiwa na miezi saba kwa sababu ya kazi ngumu alizokuwa akifanya.
Pia, anaeleza mimba tatu alizobeba ziliharibika bila yeye kujua sababu.
“Changamoto kubwa ya Wasukuma unapoolewa huku lazima ukae ukweni na utafanya kazi zote wala hawajali kama wewe bado mdogo. Wanachoamini ukishaolewa wewe ni mtu mzima,” anasisitiza.
Anashauri jamii kuendelea kuwapa fursa ya elimu watoto wao kwani ndio msingi wa mabadiliko ya kifikra, mila na tamaduni na kwamba itamwezesha kuwa chachu ya maendeleo.
Mhudumu wa afya ngazi ya jamii Kijiji cha Chasalawi, Nyanjige Makamba, anasema watoto wengi wanaolewa chini ya umri wa miaka 18 kwa sababu ya tamaa ya wazazi kwa kutaka kupata mahari.
Anashuhudia kuwa mtoto wa mdogo wake alimaliza darasa la saba na kwa kuwa hakufaulu kwenda sekondari, wazazi waliamua aolewe.
“Wazazi wanachojali ni mahari tu, sio umri wala changamoto afya ambazo mabinti zao wanaweza kupata wakati wa uzazi,” anasema Makamba.
Anasema mdogo wake kwa kushirikiana na mumewe hawakuwa na ng’ombe hivyo, waliamua kumuozesha binti yao mwenye umri wa miaka 15 ili wapate ng’ombe 10.
Pia anaeleza wazazi hao hawawatendei haki watoto wao kwani bado ni wadogo na hawawezi kujiamulia.
Anafafanua kwa sababu ya binti anayeolewa kukaa ukweni kwa ajili ya uangalizi wa karibu sambamba na kusaidia kazi za nyumbani, na kwamba yeye na mumewe wanaruhusiwa kujitegemea akifikisha miaka 25 au akiwa na watoto kuanzia wawili.
Makamba anasema hali hiyo huwafanya mabinti hao kuishi maisha ya mateso, kunyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili na kiakili.
Naye, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwamahega, Selemani Nhalima anasema mwamko mdogo wa elimu kwa wazazi huchangia watoto wa kike kuolewa katika umri ambao wanapaswa kuwa shuleni.
Nhalima anasema msukumo mkubwa wa wazazi ni kuwapatia elimu watoto wa kiume na watoto wa kike wakitakiwa kuolewa ili kuwaingizia kipato na kujikwamua dhidi ya umasikini.
“Mtoto wa kike kwa kabila letu anaonekana hana thamani kama mtoto wa kiume, wazazi wanadhani kwamba mtoto wa kike akisoma atakuwa jeuri na kujifunza tabia mbaya. Kinachotakiwa ni kuendelea kutoa elimu kwa wazazi,” anasema.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Chasalawi, Mugalula Kasululu anasema vitendo hivyo huanzia kwa wazazi kuwakataza watoto wao kujaza majibu sahihi kwenye mitihani ya kumaliza elimu ya msingi ili wasifaulu.
“Tunapata watoto wengi wazuri, unakuta wanafanya vizuri katika mitihani yote ya ndani na ya mkoa, lakini siku moja au mbili kabla ya mtihani wa kumaliza kuanza, mzazi anamshawishi mtoto ajaze madudu na kumtolea mfano hasi kuhusu watoto wenzao waliosoma na kukosa ajira,” anasema Mwalimu Mugarula.
Anasema hali hiyo huwafanya watoto kutoendelea na masomo na baada ya kukaa nje ya mfumo wa elimu, huamua kuwaozesha.
Anatoa wito kwa wadau kuendelea kutoa elimu kwa wazazi na wanajamii hao kuwapatia haki ya msingi watoto hao.



