Waajiri wapewa somo kuboresha mifumo ya taarifa

MWANZA; Waajiri wametakiwa kuhakikisha wanaweka mifumo madhubuti ya kuzuia na kushughulikia udhalilishaji, unyonyaji na ukatili wa kingono katika maeneo ya kazi, ikiwemo kuweka sera, kamati maalumu na njia salama za kutoa taarifa.

Wito huo umetolewa leo, Septemba 23, 2026, mkoani Mwanza, wakati mashirika yasiyo ya kiserikali yakijengewa uwezo kuhusu namna ya kuzuia udhalilishaji, unyonyaji na ukatili wa kingono, kuboresha mifumo ya utoaji taarifa, kuhimiza uwajibikaji na kuwezesha manusura kupata huduma na msaada.

Akizungumza baada ya elimu hiyo, Mtaalamu wa Jinsia kutoka Tanzania Bora Initiative, Sima Bateyunga, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa maonesho ya sanaa shirikishi unaolenga kutoa elimu kuhusu namna ya kuzuia udhalilishaji wa kingono mahali pa kazi.

Sima amesema sheria za Tanzania zinaelekeza kuwepo kwa mazingira salama ya kazi, hivyo kila mwajiri anapaswa kuhakikisha watumishi wanafanya kazi katika mazingira yasiyo na vitendo vya udhalilishaji.

Ameshauri waajiri kuweka mifumo rafiki ya utoaji taarifa, ikiwemo sera, kanuni na kamati maalumu zitakazoshughulikia malalamiko ya udhalilishaji katika maeneo ya kazi.

Amesema elimu hiyo imetolewa kupitia sanaa shirikishi, iliyoandaliwa na Tanzania Bora Initiative (TBI), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na Kuckuck Production.

Amesema wameamua kutumia sanaa shirikishi kwa kuwa suala hilo ni nyeti na mara nyingi halitambuliki kwa urahisi, hali inayosababisha watu wengi kuathirika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button