Watanzania wanaorejea Afrika Kusini kutibiwa bure

DAR ES SALAAM: HOSPITALI ya Rufaa ya Amana imeanzisha programu maalumu ya kuwasaidia Watanzania wanaorejea nchini kutoka Afrika Kusini kwa kutoa huduma za matibabu ya meno pamoja na ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia.
Daktari Kiongozi wa Hospitali ya Amana, Dk Mafele Ihoyelo, amesema mpango huo umeanzishwa baada ya kubaini baadhi ya Watanzania wanaorejea kutoka Afrika Kusini wakiwa na changamoto za meno, huku wengine wakihitaji msaada wa kisaikolojia ili waweze kuanza maisha mapya nchini.
Amesema huduma hizo zinalenga kurejesha afya ya kinywa kwa wanaokabiliwa na changamoto za meno, huku huduma za kisaikolojia zikilenga kuwasaidia wanaohitaji kurejesha matumaini na kuimarisha afya yao ya akili.

“Programu hiyo itatekelezwa kwa njia ya mtandao na inalenga kuwasaidia watu 100 katika awamu ya kwanza,” amesema.
Hospitali hiyo pia imezihimiza taasisi na wadau mbalimbali kujiunga na programu hiyo na kushirikiana katika kuwafikia watu wengi zaidi.
Kwa upande mwingine, Mohamed Msangi, Mtanzania anayeishi Pretoria/Johannesburg nchini Afrika Kusini, amesema Watanzania wanaorejea nchini wanahitaji kupokelewa vizuri na kusaidiwa kuanza maisha mapya badala ya kukumbana na masimango.

Msangi amesema bado kuna idadi kubwa ya Watanzania waliopo Afrika Kusini wanaohitaji kurejea nchini, lakini baadhi yao wamekuwa na hofu kuhusu namna watakavyopokelewa na kuanza maisha baada ya kukaa huko kwa muda mrefu.
Amesema baadhi ya Watanzania wameishi Afrika Kusini kwa zaidi ya miaka 15 hadi 32, huku wengine wakiwa wamejikita katika biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi, hivyo wanahitaji mazingira yatakayowawezesha kutumia ujuzi na uzoefu wao wanaporejea nchini.
Amesema hadi sasa Watanzania 543 wamekwisharejea nchini kupitia mpango huo, huku wengine 1,500 wakitarajiwa kurejea katika awamu zinazofuata. Wanaorejea wanajumuisha akina mama, watoto, vijana na wazee.
Kwa mujibu wa Msangi, changamoto za meno na afya ya kisaikolojia ni miongoni mwa mahitaji yaliyoonekana kwa baadhi ya wanaorejea, hivyo ushiriki wa Hospitali ya Amana na wadau wengine unaweza kusaidia kuwawezesha kuanza upya maisha yao nchini.



