Abri achangia mabati Usolanga

IRINGA: Ujenzi wa nyumba ya muhudumu wa afya katika Zahanati ya Usolanga, wilayani Iringa unatarajiwa kupiga hatua baada ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Arif Abri, kuchangia mabati 30.

Pamoja na msaada huo utakaosaidia kuimarisha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani, kada huyo wa CCM ametoa msaada wa kompyuta moja kwa matumizi ya Zahanati hiyo.

Diwani wa Kata ya Malengamakali, Stephano Mkisi, amesema nyumba hiyo ni sehemu muhimu ya jitihada za wananchi kuhakikisha wahudumu wa afya wanakuwa na mazingira bora ya kuishi karibu na kituo chao cha kazi.

“Mpango huu unalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma wakati wowote, hususan kwa wagonjwa wanaohitaji msaada wa haraka nje ya muda wa kawaida wa kazi,” amesema.

Amesema msaada huo wa Abri umeongeza nguvu katika ujenzi wa nyumba hiyo ambayo tayari ilikuwa imefikia hatua ya kuezekwa wakati wananchi walipowasilisha mahitaji yao kwa viongozi na wadau wa maendeleo.

Mkisi, amesema ujenzi wa nyumba hiyo ni miongoni mwa mahitaji muhimu yaliyotambuliwa na wananchi kwa lengo la kuboresha huduma katika zahanati hiyo.

Mabati hnpamoja na kompyuta hiyo yamekabidhiwa kwa niaba ya Abri na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Arnold Mvamba, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho.

Akizungumza katika mkutano huo, Mvamba amesema serikali ndiyo mdau mkuu wa maendeleo, lakini ushiriki wa wananchi, viongozi na wadau wengine ni muhimu katika kuharakisha utekelezaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi.

Mvamba amesema msaada huo unatokana na ahadi iliyotolewa na Abri wakati wa ziara yake Usolanga, ambapo wananchi walieleza changamoto zinazowakabili katika huduma za afya na uhitaji wa vifaa vya teknolojia.

Amesema msaada huo unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, wananchi na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto za huduma za kijamii.

Licha ya msaada huo kuwa hatua muhimu ya ujenzi huo amesema, bado ushirikiano wa wananchi unahitajika ili kukamilisha nyumba hiyo na kuhakikisha inatumika kwa lengo lililokusudiwa.

Aidha Mvamba amewataka wananchi kuendelea kuzingatia tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu mwenendo wa mvua na kuchukua hatua stahiki kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button