THRDC yakemea ukatili kwenye jamii
DAR ES SALAAM: MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeishauri Serikali kuchukua hatua za kuridhia na kuweka katika sheria za ndani mikataba ya kimataifa inayolenga kulinda watu dhidi ya kutoweka kwa kulazimishwa na vitendo vingine vya kikatili au vya udhalilishaji vinavyoendelea katika jamii.
Akizungumza kupitia tamko kwa vyombo vya habari, Mratibu wa Taifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema Tanzania inapaswa kujiunga na kutekeleza kikamilifu Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya vitendo visivyo vya kibinadamu.
Olengurumwa amesema Tanzania inapaswa pia kuendelea na mchakato wa kuridhia na kutekeleza Mkataba wa Kimataifa wa Kulinda Watu Wote Dhidi ya Kutoweka kwa Kulazimishwa ambao Tanzania ilisaini Septemba 29, 2008.
Kwa mujibu wa THRDC, utekelezaji wa mikataba hiyo unapaswa kuambatana na kutungwa kwa sheria zinazotambua mateso na kutoweka kwa kulazimishwa kama makosa tofauti ya jinai, kuweka uwajibikaji wa viongozi wa juu kwa vitendo vya walio chini yao, pamoja na kuhakikisha waathirika wanapata tiba, fidia na ulinzi unaostahili.
Aidha, THRDC imeitaka Serikali kupiga marufuku kuweka watu kwa muda mrefu katika seli za polisi na kuanzisha vituo maalumu vya kuwaweka mahabusu kabla ya kesi chini ya Jeshi la Magereza.
Olengurumwa amesema kizuizi cha polisi kinapaswa kuwa kwa muda unaoruhusiwa kisheria, ambapo mshukiwa anapaswa kufikishwa mbele ya mahakama yenye mamlaka au kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Pale ambapo kuendelea kuwekwa kizuizini kumeidhinishwa kisheria, mtu huyo anapaswa kuhamishiwa katika kituo maalumu cha mahabusu chini ya Jeshi la Magereza.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa seli za polisi kwa ujumla hazijaandaliwa kwa ajili ya kuwahifadhi watu kwa muda mrefu na zinaweza kukosa usafi, hewa ya kutosha, chakula, huduma za matibabu na sehemu nzuri za kulala. Hivyo hali hiyo inaweza kuathiri utu wao.



