Kadogosa ataka ushirikiano kuimarisha ujenzi

DODOMA: WAZIRI wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, amesema atashirikiana kwa karibu na viongozi na watumishi wa wizara hiyo kuhakikisha miradi inayotekelezwa katika Sekta ya Ujenzi inatekelezwa kwa weledi na ufanisi, kwa lengo la kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali katika kuendeleza miundombinu nchini.
Kadogosa ameyasema hayo leo, Oktoba 2, 2026, katika Ofisi za Wizara ya Ujenzi, Mtumba jijini Dodoma, mara baada ya kuwasili na kukabidhiwa rasmi Ofisi na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Septemba 27, 2026.

Amesema yupo tayari kujifunza, kupokea maoni na ushauri kutoka kwa viongozi, watumishi na wadau mbalimbali kuhusu namna bora ya kuendeleza na kukuza Sekta ya Ujenzi nchini, akisisitiza kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya taifa.
“Niwaeleze kuwa Ofisi yangu ipo wazi kwa yeyote mwenye maoni na ushauri wa kuboresha Sekta yetu. Mlango upo wazi, tushirikiane kwa pamoja kuinua Sekta hii,” amesema Kadogosa.
Aidha, Kadogosa amepongeza namna wizara, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ilivyojipanga kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazotarajiwa kunyesha nchini.

Amesisitiza umuhimu wa wakala huo kuendelea kuchukua tahadhari na hatua stahiki za kuimarisha usalama na uendelevu wa miundombinu ya barabara na madaraja, hususan katika kipindi cha mvua.
Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na sasa Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Ulega, amewataka watumishi wa Wizara ya Ujenzi kumpa ushirikiano wa kutosha Waziri mpya ili wizara hiyo iendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kusonga mbele katika ujenzi wa taifa.

Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, Katibu Mkuu, Balozi, Mhandisi Aisha Amour, Naibu Katibu Mkuu, Dk. Charles Msonde, Menejimenti ya Wizara, Wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara pamoja na baadhi ya watumishi wa Wizara.



