COP12 kuibua fursa mpya uchumi wa buluu

DAR ES SALAAM: TANZANIA inatarajia kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaoanza leo, Oktoba 6, 2026, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na nchi wanachama kutumia rasilimali za Bahari ya Hindi kwa ajili ya kukuza Uchumi wa Buluu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Richard Muyungi, amesema mkutano huo umewakutanisha zaidi ya washiriki 1,460 kutoka nchi 10 wanachama wa Mkataba wa Nairobi.
Amesema ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi una rasilimali na shughuli mbalimbali za kiuchumi, zikiwemo za utalii, uvuvi, usafirishaji na nishati, ambazo zina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi za ukanda huo.
Kwa mujibu wa Dk Muyungi, COP12 pia inalenga kuwashirikisha vijana katika kutambua na kutumia fursa zinazotokana na bahari, ikiwa ni pamoja na fursa za ajira na ujasiriamali.
Amesema vijana watapatiwa ujuzi na mbinu za kutumia fursa hizo kujipatia kipato na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi wa buluu, hatua itakayochangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Aidha, amesema wafanyabiashara na wajasiriamali watapata fursa ya kujifunza na kutambua maeneo mbalimbali ya uwekezaji yanayotokana na uchumi wa buluu.
“Wengi tunafahamu kwenye bahari kuna aina mbalimbali za mazao. Kwa mfano, tuna samaki na wavuvi wana nafasi ya kutumia vizuri bahari kuvua samaki kwa ajili ya biashara na chakula. Pia tuna shughuli za utalii zinazotuingizia kipato na tunaweza kupata gesi asilia kupitia bahari,” amesema.
Dk Muyungi pia amesema wanawake, hususan wanaotoka maeneo ya pwani ya Zanzibar, wataendelea kunufaika na fursa zitakazotokana na COP12 kupitia uwezeshaji wa shughuli zao za kiuchumi na upanuzi wa soko la kilimo cha mwani.
Amesema mwani ni miongoni mwa mazao yanayochangia katika kuongeza kipato cha wananchi na taifa, hivyo wanawake wajasiriamali wanaojihusisha na kilimo hicho watapata elimu na ujuzi wa kuwawezesha kuboresha uzalishaji na kuongeza tija.
Ameongeza kuwa ushiriki wa vijana, wanawake na wafanyabiashara katika fursa za uchumi wa buluu ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali za bahari zinatumika kwa tija na kuchangia maendeleo endelevu ya Tanzania.



