Tanzania yasisitiza suluhisho la kudumu kwa Wakimbizi

GENEVA: Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, ameunga mkono Dira ya Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Barham Salih, ya “50 kufikia 35”, inayolenga kupunguza kwa nusu idadi ya wakimbizi duniani ifikapo mwaka 2035.
Ayoub alitoa kauli hiyo jana, Oktoba 13, 2026, wakati akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 77 wa Kamati Tendaji ya UNHCR uliofanyika jijini Geneva, Uswisi.
Akichangia mjadala wa mkutano huo, alisema Tanzania imeendelea kuchukua hatua za kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi, ikiwemo kushiriki katika mchakato wa kuwarejesha wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) nchini mwao.

Alisema Serikali pia imeshatoa uraia kwa zaidi ya wakimbizi 160,000 wa Burundi walioingia Tanzania mwaka 1972, huku akibainisha kuwa kundi lililosalia halitapewa uraia, bali Serikali itaendelea kutafuta suluhisho jingine la kudumu kwao.
Mhe. Ayoub aliitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza rasilimali kwa ajili ya huduma muhimu kwa wakimbizi, ikiwemo afya, elimu na chakula, pamoja na kutoa msaada wa kitaalamu na kifedha katika zoezi la uhakiki wa wakimbizi wa Burundi.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa UNHCR, Barham Salih, ameipongeza Tanzania kwa juhudi zake za kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi na kuahidi kuendelea kutoa msaada wa kitaalamu.

Katika hatua nyingine, Ayoub alikutana na viongozi mbalimbali wa UNHCR, akiwemo Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Masuala ya Hifadhi, Edem Wosornu, na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki, Maziwa Makuu Kusini na Pembe ya Afrika, Dk Mamadou Balde.
Katika mazungumzo hayo, alihimiza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na UNHCR katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi kutoka Burundi na DRC.

Aidha, aliiomba UNHCR kufadhili zoezi la uhakiki wa wakimbizi wa Burundi na kuongeza ufadhili wa elimu ya juu kwa wakimbizi kutoka DRC.
Kwa upande wake, Wosornu aliahidi kulifanyia kazi ombi la Tanzania kuhusu elimu ya juu na kuendelea kushirikiana na Tanzania, Burundi na DRC katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi.



