Watalii wa misitu waongezeka nchini

DAR ES SALAAM: Idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za misitu nchini imeongezeka kutoka chini ya 200 mwaka 2015 hadi zaidi ya 390,000 kwa mwaka, hatua inayoashiria kuongezeka kwa shughuli za utalii.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umesema ongezeko hilo linachangiwa na juhudi za kuboresha uhifadhi na kuendeleza utalii wa misitu.
Ofisa Uhifadhi TFS, Yusuph Tango, ametoa takwimu hizo leo Oktoba 13, 2026 wakati akizungumza kuhusu awamu ya tisa ya ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Mazingira GEF (GEF-9) ambapo alisema miradi inayofadhiliwa na mfuko huo imechangia kukuza sekta hiyo na kuongeza thamani ya rasilimali zake.
Amesema utalii wa misitu ulikuwa bado mpya mwaka 2015 wakati Tanzania ikijulikana zaidi kwa vivutio vya utalii wa wanyamapori.
“Tulipoanza mwaka 2015, idadi ya watalii waliotembelea hifadhi za misitu ilikuwa chini ya 200 kwa mwaka. Kama mnavyojua, nchi yetu inatambulika zaidi kwa utalii wa wanyamapori, lakini utalii wa misitu ulikuwa bado ni dhana mpya,” amesema Tango.
Amesema idadi hiyo imeongezeka hadi zaidi ya watalii 390,000 kwa mwaka, huku akiitaja miradi iliyofadhiliwa na GEF kuwa miongoni mwa hatua zilizochangia maendeleo hayo.
Ameeleza kuwa miradi hiyo imesaidia kuboresha hali na usimamizi wa baadhi ya misitu, ikiwemo kuipandisha hadhi na kuwa hifadhi za misitu ya asili hatua iliyowezesha kuanzishwa na kuendelezwa kwa shughuli za utalii sambamba na uhifadhi.
Ameongeza kuwa maendeleo hayo yanaipa Tanzania fursa ya kuongeza vivutio vya utalii nje ya wanyamapori huku yakichangia matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na kulinda bioanuwai.
Tango amesema TFS imekuwa ikinufaika na ufadhili wa GEF tangu mwaka 2007 kupitia awamu mbalimbali, zikiwemo GEF-4, GEF-5 na GEF-6, na sasa inaangalia fursa za ufadhili kupitia GEF-9 ili kuimarisha zaidi shughuli za uhifadhi.
Ameeleza kuwa jukumu la TFS ni kusimamia na kuhifadhi rasilimali za misitu na nyuki kwa njia endelevu hivyo ufadhili zaidi utasaidia kuendeleza shughuli zinazolingana na malengo ya uhifadhi, ikiwemo utalii katika hifadhi za misitu na nyuki.
Amefafanua TFS inatafuta fursa za kushirikiana na wadau mbalimbali kuandaa mapendekezo ya miradi yanayozingatia vipaumbele vya mazingira vya Tanzania na kukidhi vigezo vya ufadhili wa GEF.
Mazungumzo ya kitaifa kuhusu GEF-9 yanalenga kuwakutanisha wadau kujadili fursa za ufadhili, kujifunza kutokana na utekelezaji wa miradi iliyopita na kubainisha maeneo ya kipaumbele pamoja na mawazo ya miradi inayoweza kupewa ufadhili nchini.
Tango amesema upatikanaji wa ufadhili zaidi kupitia GEF-9 utaipa TFS fursa ya kuendeleza mafanikio yaliyopatikana, kuimarisha uhifadhi wa misitu na kuongeza mchango wa rasilimali za misitu na nyuki katika maendeleo ya Tanzania.



