Rais Samia kubariki maadhimisho taasisi za kiraia

DAR ES SALAAM: Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 70 ya usajili, usimamizi na udhibiti wa taasisi za kiraia yatakayofanyika Oktoba 27 hadi 29, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema maadhimisho hayo yenye kaulimbiu isemayo ‘Jumuiya za Kiraia ni Msingi wa Umoja, Mshikamano na Maendeleo ya Taifa’, yanalenga kuimarisha amani na usalama wa nchi, mshikamano wa kitaifa na ushirikiano kati ya taasisi za kiraia.

Amesema kupitia Ofisi ya Msajili wa Asasi za Kiraia, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi ina jukumu la kusajili, kusimamia na kudhibiti taasisi hizo kwa mujibu wa sheria, huku maadhimisho hayo yakitoa fursa kwa wadau kujadili namna ya kuboresha utendaji wake.

Amesema maadhimisho hayo yatakuwa jukwaa la viongozi wa taasisi za kiraia, taasisi za dini na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na kuweza kubadilishana mawazo, kutoa maoni na mapendekezo kuhusu sheria, sera na mifumo inayosimamia taasisi hizo.

Amesema mada zitakazojadiliwa ni pamoja na majukumu na wajibu wa ofisi ya usajili wa jumuiya, haki na wajibu wa jumuiya zilizosajiliwa, fursa za uwekezaji, mifumo ya kodi na elimu ya kodi, mifumo ya kifedha na elimu ya kifedha na wajibu wa taasisi hizo katika kulinda amani.

Amesema maadhimisho hayo yatatumika kutathmini utendaji wa taasisi zilizosajiliwa, ikiwamo kubaini taasisi ambazo hazifanyi kazi kwa mujibu wa sheria na changamoto zinazohitaji kutatuliwa.

Amesema tathmini hiyo itasaidia kubaini hatua zilizopigwa katika kipindi cha miaka 70, changamoto zilizopo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuboresha usimamizi wa taasisi hizo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button