Bodi yajadili maendeleo uhuishaji, utendaji TAZARA

DAR ES SALAAM; Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na-Zambia (TAZARA) imekutana jijini Dar es Salaam kwa masuala mbalimbali ikiwemo kupokea na kujadili taarifa na mapendekezo kutoka kamati zake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Uhusiano wa Umma wa TAZARA, Conrad Simuchile, kikao hicho cha 123 kilifanyika Oktoba 12, 2026 kwenye Ofisi Kuu za mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Taarifa imesema kikao pia kilipitia maendeleo ya uhuishaji, utendaji kazi na ufadhili wa huduma katika kipindi cha mpito cha ukodishaji (concession).
“Kikao kiliongozwa na Mwenyekiti Prof Godius Kahyarara, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mwenyekiti mwenza Mhandisi Fredrick Mwalusaka, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi na Logistiki ya Jamhuri ya Zambia.

“Wakurugenzi wengine waliohudhuria Peter Noni (Tanzania), Irene Lumbwe (Zambia) na Lazarous Mwelwa (Zambia).
“Bodi ilipokea na kujadili taarifa na mapendekezo kutoka kamati zake, ikiwemo maendeleo ya mpango wa uhuishaji, utendaji wa mamlaka kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2026.
“Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa 2026/2027–2030/2031 na bajeti ya shirika ya mwaka 2026/2027,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa imesema Bodi ilipitia utekelezaji wa Mkataba wa Ukodishaji kati ya TAZARA na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), unaotoa uwekezaji wa Dola za Marekani Bilioni 1.4 kwa ajili ya uhuishaji.
“Ilijadili maendeleo ya mkodishaji katika kuandaa vifaa, kufanya tafiti za miundombinu na shughuli nyingine za maandalizi tangu Mkataba uliposainiwa Septemba 2025.

“Bodi pia ilijadili matakwa yaliyobaki ambayo lazima yatimizwe kabla ya mkataba kuanza kutekelezwa kikamilifu, pamoja na mipango ya kulinda mali za reli na kuendelea kutoa huduma wakati wa kipindi cha mpito.
“Bodi ilielekeza Menejimenti kuimarisha usimamizi wa ukodishaji kupitia timu maalum ya wataalamu, uhakiki wa mali za reli, uwasilishaji wa taarifa za kiufundi na kifedha kwa uwazi, na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa utekelezaji wa ahadi za uwekezaji, utendaji kazi, viwango vya usalama na matakwa ya kimkataba ya mkodishaji,” imesema taarifa hiyo.
“Bodi iliidhinisha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Menejimenti wa 2026/2027–2030/2031, unaounganisha urejeshaji wa uendeshaji wa TAZARA na uendelevu wa kifedha wa muda mrefu na utekelezaji wa Mkataba wa Ukodishaji na CCECC,” imeeleza.



