SACCOS zatakiwa kutumia AI kurejesha imani ya wananchi

DAR ES SALAAM: VYAMA vya akiba na mikopo (SACCOS) vimetakiwa kutumia Akili Unde na teknolojia za kisasa kuboresha usimamizi, kuongeza ufanisi na kurejesha imani ya wananchi, huku vikivutia vijana kujiunga na sekta hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam Oktoba 14, 2026, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dk Benson Ndiege, amesema matumizi ya teknolojia na usimamizi bora ni muhimu katika kuimarisha utendaji wa SACCOS na kukabiliana na changamoto zilizokuwa zikidhoofisha imani ya wanachama.
Amesema hayo wakati wa Kongamano la 26 la Kimataifa la Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Barani Afrika (SACCA Congress 2026), linalofanyika Oktoba 11 hadi 16, Dar es Salaam, likiwa na washiriki kutoka zaidi ya nchi 28.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Fares Muganda, amesema AI inaweza kurahisisha mawasiliano, kuboresha huduma na kuvutia vijana kwa kuhakikisha wanapata huduma za kifedha kwa urahisi.
Wakati huo huo, Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT), Hassani Mnyone, amesema kongamano hilo linaitangaza Tanzania kimataifa na kutoa fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara wa usafiri, malazi na chakula.
Amesema mwaka 2025, SACCOS zilikuwa na mali zenye thamani ya takribani Sh trilioni 1.6 na wanachama wapatao milioni mbili, huku zikiendelea kusaidia upatikanaji wa mikopo na kukuza shughuli za kiuchumi katika jamii.
Kongamano hilo linatarajiwa kuimarisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kuendeleza SACCOS imara na endelevu barani Afrika.
Mwisho



