Mradi wa Maji wa Rwakajunju wafikia asilimia 79

KAGERA: UJENZI wa Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Rwakajunju, wilayani Karagwe, mkoani Kagera, umefikia asilimia 79, huku huduma ya maji safi na salama ikitarajiwa kuanza kutolewa mwishoni mwa Desemba mwaka huu.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi, Mathew Kundo amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 63 ni mkombozi kwa wananchi zaidi ya 350,000 wa wilaya hiyo, kwa kuwa utaboresha upatikanaji wa maji na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Kundo alisema kukamilika kwake kutarahisisha upatikanaji wa maji kwa wananchi na kunufaisha sekta mbalimbali, ikiwemo viwanda, kupitia ongezeko la uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

“Mradi huu unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 63. Nimepata maelezo kutoka kwa wasimamizi kuhusu kazi zilizokamilika na zinazoendelea. Nimejionea maendeleo yaliyofikiwa, ambayo yanaanza kuleta matumaini kwa wananchi waliokuwa wakisubiri huduma hii kwa muda mrefu,” alisema.

Aliongeza kuwa ziara za awali zilikuwa zikifanyika wakati hali ya mradi haikuwa ya kuridhisha, lakini kwa sasa matumaini ya wananchi kupata maji yameanza kuonekana.

Kundo alisisitiza kuwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo anapaswa kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilishwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, ili wananchi wa Omurushaka waanze kupata huduma ya maji safi na salama kama ilivyopangwa.

Aidha, alimtaka msimamizi wa Mamlaka ya Bonde kuhakikisha chanzo cha maji kinachotumika katika mradi huo kinalindwa dhidi ya shughuli zinazoweza kuharibu mazingira na kuhatarisha upatikanaji wa maji katika siku zijazo.

Alisema utunzaji wa chanzo cha maji ni muhimu katika kuhakikisha mradi unakuwa endelevu na unaendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, msimamizi wa mradi huo, Evodius Byeyanga, alisema kazi mbalimbali zinaendelea kutekelezwa ili kuhakikisha mradi unakamilika. Alitaja shughuli zinazoendelea kuwa ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji na utandazaji wa mabomba hadi mji wa Omurushaka.

Byeyanga alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Aprili 2023 na awali ulitarajiwa kukamilika Desemba 2025. Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, muda wa kukamilika kwake uliongezwa hadi Julai 2027.

Alisema mradi huo unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama, kupunguza adha ya wananchi kutafuta maji na kuweka mazingira bora kwa ukuaji wa shughuli za kijamii na kiuchumi katika Wilaya ya Karagwe na maeneo mengine yatakayohudumiwa.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza upatikanaji wa maji katika miji ya Kayanga na Omurushaka kutoka asilimia 65 hadi asilimia 100

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button