‘Mradi hewa ya kaboni umeleta neema kwa familia’

KATAVI; Wananchi wa Kata ya Katuma, Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, wamesema mradi wa biashara ya hewa ya kaboni umesaidia kupunguza changamoto ya kuchangishana fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo afya, elimu, miundombinu, ofisi za vijiji na nyumba za watumishi.

Wametoa kauli hiyo wakati wakizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni kwenye kata hiyo.

Wamesema manufaa hayo yanaonesha namna uhifadhi wa mazingira unavyoweza kuwa chanzo cha fedha za kuboresha huduma na maisha ya wananchi.

Kwa upande wake Waziri Masauni amesema serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi ili kuweka mazingira wezeshi ya usimamizi wa biashara ya hewa ya kaboni, ikiwemo utaratibu wa mgawanyo wa mapato yatokanayo na miradi hiyo.

Masauni amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inaelekeza biashara ya hewa ya kaboni kuwa chachu ya uhifadhi wa mazingira, uzalishaji wa ajira na ukuaji wa uchumi.

Ameongeza kuwa Wilaya ya Tanganyika ina fursa kubwa ya kunufaika na biashara hiyo, huku wananchi wanaomiliki maeneo yenye miradi hiyo wakipata nafasi ya kunufaika na mapato yake akiwataka wananchi kuendelea kushiriki katika shughuli za uhifadhi kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Serikali.

Awali, Diwani wa Kata ya Katuma, Daudi Kalele, aliiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa wauguzi katika Kituo cha Afya Katuma, kinachotarajiwa kuanza kutoa huduma Novemba Mosi mwaka huu. Katika ziara hiyo, Masauni alitembelea kituo hicho, kupokea taarifa ya mradi na kugawa vyandarua pamoja na vifaa tiba.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button