Vitambulisho milioni 21.5 vyafikishwa kwa wananchi

DODOMA: Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesajili mafanikio ya utoaji wa Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) milioni 23.7, huku vitambulisho zaidi ya milioni 21.5 vikishasambazwa kwa wananchi, hatua inayoakisi maendeleo ya mifumo ya utambuzi wa raia nchini.

Mafanikio hayo yamewasilishwa leo Oktoba 20 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, wakati akiwasilisha taarifa za utendaji wa NIDA na Chuo cha Zimamoto na Uokoaji cha Chogo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, NIDA imezalisha NIN 23,718,060 na vitambulisho 21,526,594, ambapo 21,515,793 vimesambazwa kwa wananchi.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na mamlaka hiyo ni kuunganisha taasisi 152 za umma na binafsi kwenye kanzidata yake, kuanza kutumia teknolojia ya Laser Engraving katika uzalishaji wa vitambulisho na kuboresha moduli 24 za mfumo wa usajili na utambuzi.

Hatua hizo zinaenda sambamba na juhudi za kuimarisha mifumo ya utambulisho na kurahisisha upatikanaji wa huduma zinazotegemea taarifa sahihi za utambuzi wa watu.

Katika eneo la usalama na uokoaji, Chuo cha Zimamoto na Uokoaji cha Chogo, kilichopo Handeni mkoani Tanga, kimeendesha kozi 57 tangu mwaka 2016, zilizowajengea uwezo maafisa na askari 5,934.

Mafunzo hayo yanahusisha kuzuia na kuzima moto, shughuli za uokoaji, huduma ya kwanza na matumizi ya vifaa vya kukabiliana na majanga.

Aidha, chuo hicho kimeshiriki katika matukio 20 ya kuzima moto na uokoaji katika maeneo ya Segera, Kabuku na Mkata, na kufanikiwa kuokoa majeruhi 102.

Kamati ya Bunge imepongeza juhudi za NIDA kuboresha huduma zake na kusisitiza umuhimu wa Chuo cha Zimamoto na Uokoaji cha Chogo kuendelea kuimarisha miundombinu yake ili kuongeza ufanisi wa mafunzo na maandalizi ya kukabiliana na majanga.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button