Wataalamu manunuzi watakiwa kulinda fedha za umma

DAR ES SALAAM: WATAALAMU wa manunuzi na ugavi wametakiwa kuimarisha uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kudhibiti upotevu wa fedha za umma na kuhakikisha kila fedha inayotumika kununua bidhaa na huduma inatoa thamani inayostahili.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Deogratius Luswetula, wakati wa mahafali ya 15 ya wataalamu wa manunuzi na ugavi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambako alisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria, maadili na taratibu za taaluma hiyo.
Luswetula amesema wataalamu hao wana nafasi muhimu katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuepuka vitendo vya udanganyifu pamoja na mgongano wa maslahi vinavyoweza kuathiri ufanisi wa mifumo ya ununuzi.

Amesema kuimarisha maadili katika taaluma hiyo ni miongoni mwa hatua zinazoweza kusaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha, kuboresha utoaji wa huduma na kupunguza mianya ya upotevu wa rasilimali za umma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (PSPTB), Jacob Kibona, amesema bodi hiyo inaendelea kuboresha mitaala, kutoa mafunzo endelevu na kuimarisha usimamizi wa taaluma ili kuongeza weledi na ufanisi katika sekta ya manunuzi na ugavi.

Kibona amesema juhudi hizo zinalenga kuhakikisha wataalamu wanakuwa na maarifa na uwezo unaokidhi mahitaji ya taaluma, huku wakizingatia viwango vinavyotakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma Serikalini, Alex Haraba, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na bodi, vyuo na waajiri kuongeza idadi ya wataalamu wenye sifa na kuhakikisha nafasi za kazi za manunuzi zinajazwa na watumishi waliokidhi vigezo vya kitaaluma.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha mifumo ya ununuzi wa umma na kuhakikisha taasisi zina wataalamu wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Kwa upande wake, mhitimu wa programu hizo, Ismael Kagungu, amesema wahitimu wamejipanga kutumia maarifa waliyoyapata kuimarisha uwazi, ushindani na matumizi bora ya fedha za umma katika maeneo yao ya kazi.



