I&M Bank Tanzania sasa yajinafasi Soko la Hisa

DAR ES SALAAM: Benki ya I&M Tanzania imeorodhesha rasmi dhamana yake ya uwekezaji ya I&M Hatua Bond katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), baada ya kupokea maombi ya uwekezaji yenye thamani ya Sh bilioni 161.38 dhidi ya lengo la awali la Sh bilioni 20, sawa na usajili wa asilimia 806.92.

Uorodheshaji huo ulifanyika Oktoba 15, 2026, katika ofisi za DSE jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na wawakilishi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), viongozi wa I&M Bank Tanzania, iTrust Finance Limited pamoja na wadau mbalimbali wa soko la mitaji nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Bank Tanzania, Zahid Mustafa, amesema mwitikio mkubwa wa wawekezaji unaonesha imani waliyonayo kwa benki hiyo, mkakati wake wa ukuaji na fursa zilizopo katika uchumi wa Tanzania.

Amesema fedha zitakazopatikana kupitia dhamana hiyo zitasaidia kuongeza uwezo wa benki kutoa mikopo kwa wafanyabiashara, wateja wa rejareja na biashara ndogo na za kati, pamoja na kuwekeza katika teknolojia na mifumo ya kidijitali.

“Hatua Bond ni dhamana ya uwekezaji ya miaka mitano inayotoa riba ya kudumu ya asilimia 13 kwa mwaka, inayolipwa kila robo mwaka, huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwa Shilingi 500,000.

“Dhamana hiyo ni sehemu ya mpango wa I&M Bank Tanzania wa kukusanya mitaji ya muda wa kati na mrefu ili kuimarisha shughuli zake za kibiashara na uwezo wa kuhudumia wateja,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama, ameipongeza I&M Bank Tanzania kwa kufanikisha mauzo na uorodheshaji wa dhamana hiyo, akieleza kuwa hatua hiyo inaongeza fursa za uwekezaji na kuchangia upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu kupitia soko la mitaji nchini.

Naye Mkurugenzi wa iTrust Finance Limited, Profesa Mohamed Warsame, ambaye ni mshauri wa muamala na dalali mdhamini wa Hatua Bond, amesema mwitikio huo unaashiria kuongezeka kwa mahitaji ya fursa za uwekezaji katika dhamana zinazotoa mapato ya kudumu, hatua inayoweza kuchangia maendeleo ya soko la mitaji nchini Tanzania.

I&M Bank Tanzania imeendelea kupanua shughuli zake za kibenki na kufikia hadhi ya Benki Daraja la Kwanza (Tier One), huku jumla ya mali zake ikivuka Shilingi trilioni moja mwaka 2026.

I&M Bank Tanzania ni sehemu ya I&M Group PLC, kundi la huduma za kibenki na kifedha linalofanya shughuli zake katika nchi za Afrika Mashariki na Mauritius, likihudumia watu binafsi, wafanyabiashara na taasisi kupitia mtandao wa matawi na huduma za kibenki kidijitali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button