Ukarabati wa samani waokoa Sh milioni 233

DAR ES SALAAM: Kampeni ya kukarabati samani zilizoharibika katika shule za msingi na sekondari za Serikali katika Kata ya Goba, Manispaa ya Ubungo, imewezesha kuokoa zaidi ya Sh milioni 233 ambazo zingetumika kununua madawati, viti na meza mpya.
Kampeni hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Jimbo la Kibamba na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki, imewezesha kukarabati jumla ya samani 2,583 katika shule za msingi na sekondari za Serikali zilizopo katika kata hiyo.
Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Stanley Mkandawile, amesema hayo leo Oktoba 24, 2026, wakati wa hafla ya kukabidhi samani zilizokarabatiwa katika Kata ya Goba.

Amesema hatua hiyo imepunguza gharama ambazo zingetumika kununua samani mpya, huku ikisaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Mkandawile amesema kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita, baadhi ya wanafunzi walilazimika kukaa chini kutokana na upungufu wa madawati, hali iliyokuwa ikiathiri mazingira yao ya kujifunzia.
Ametoa wito kwa viongozi kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya elimu katika kata hiyo, ikiwemo upungufu wa vyoo.
Kwa upande wake, Kairuki amesema samani hizo zimekarabatiwa kwa kushirikisha viongozi, walimu na vijana wenye ujuzi, hatua iliyosaidia kurejesha matumizi ya samani ambazo vinginevyo zingelazimika kubadilishwa.

Amesema jitihada za kuboresha elimu katika kata hiyo pia zinahusisha ujenzi na ukarabati wa madarasa, maabara, vyoo pamoja na vyumba vya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
“Katika kipindi cha mwaka mmoja, Serikali Kuu na halmashauri zimetenga shilingi bilioni 718 kwa ajili ya miradi ya elimu katika kata yetu. Niwapongeze mafundi waliohusika kwa kutumia ujuzi wao kurejesha samani hizi kwa gharama ndogo ikilinganishwa na kununua mpya,” amesema.
Akisoma taarifa ya hali ya elimu, Ofisa Elimu wa Kata ya Goba, Ezekiel Msingi, amesema kata hiyo ina shule saba za msingi zenye wanafunzi 12,085 na shule sita za sekondari zenye wanafunzi 4,560.
Amesema kampeni hiyo ililenga kutumia samani ambazo bado zinaweza kurekebishwa badala ya kununua mpya, hatua inayosaidia kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amewataka watendaji kuwajibika katika utekelezaji wa maagizo ya Serikali, akisema viongozi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao hawapaswi kuendelea kushikilia nafasi zao.
Msando pia amewaagiza maofisa elimu, walimu wakuu na watendaji wa kata kuhakikisha madawati yaliyoharibika yanatambuliwa na kupelekwa katika vituo vinavyohitaji kabla ya Jumatatu.
Amesema hakuna sababu ya wanafunzi kuendelea kukosa madawati wakati samani zilizopo zinaweza kurekebishwa na kutumika tena.



