Madawati msaada wa kisheria kuimarishwa magerezani

DAR ES SALAAM; WAZIRI wa Katiba na Sheria, Abdallah Ulega, ameiagiza Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Magereza kuhakikisha madawati ya msaada wa kisheria yanaanzishwa na kuimarishwa katika makao makuu ya Jeshi la Magereza, ofisi za mikoa na magereza nchini ili wafungwa na mahabusu wapate huduma hizo kwa wakati.
Aidha, amesisitiza matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika kurahisisha ufuatiliaji wa mashauri, usimamizi wa taarifa na mawasiliano baina ya taasisi zinazohusika na utoaji wa haki.
Ulega anasema maagizo hayo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata haki zao kwa mujibu wa Katiba, sheria na taratibu za nchi, bila kujali uwezo wao wa kiuchumi.

Akizungumza katika hafla ya kusaini hati ya makubaliano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhusu utoaji wa huduma za msaada wa kisheria magerezani, iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam, anabainisha kuwa haki ni msingi wa amani, usawa na maendeleo ya taifa.
Anasema hati hiyo ya makubaliano haipaswi kuwa nyaraka ya kuhifadhiwa kwenye makabati, bali inapaswa kutekelezwa kwa vitendo ili kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata taarifa sahihi kuhusu haki na wajibu wao, ushauri wa kisheria, msaada wa kuandaa nyaraka pamoja na uwakilishi mahakamani.
Ulega anasisitiza kuwa mtu anapokuwa kizuizini au gerezani bado anastahili kuheshimiwa haki zake, hivyo taasisi zinazohusika zinapaswa kuhakikisha huduma hizo zinapatikana na kutolewa kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, anasema wafungwa na mahabusu 19,511 katika mikoa saba nchini wamenufaika na huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa na Jeshi la Magereza.
Anasema huduma hizo zimetolewa katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Shinyanga, Simiyu, Ruvuma, Singida na Njombe, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha upatikanaji wa haki, kupunguza msongamano magerezani na kuongeza ufanisi wa mfumo wa haki jinai.

Katambi anafafanua kuwa huduma hizo zinatekeleza haki ya kikatiba ya kila mwananchi kujitetea au kutetewa, akibainisha kuwa Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweka msingi wa haki hiyo.
“Hatupendi kuwatunza hawa wenzetu magerezani. Hata askari hawa wanajua hatupendi tutunze wafungwa, ndiyo maana tunaendelea kusisitiza umuhimu wa kuwapatia msaada wa kisheria utakaowawezesha kuelewa mashauri yao na kutumia fursa zilizopo kisheria kutetea haki zao,” anasema Katambi.
Anasema baadhi ya watu hukumbwa na changamoto katika mashauri yao kutokana na kushindwa kujieleza vizuri, kuwasilisha nyaraka muhimu au kuunganisha ushahidi unaoweza kusaidia utetezi wao.
Katambi anaeleza kuwa msaada wa kisheria utawasaidia wafungwa na mahabusu kuelewa hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika mashauri yao, ikiwemo kutumia njia zinazotambuliwa kisheria kukata rufaa pale inapostahili.
“Upande wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tunawahakikishia tutalisimamia jambo hili usiku na mchana, kwa sababu ninafahamu litakuwa na maslahi makubwa kwa Watanzania,” anasema.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Magereza limeeleza kuwa zaidi ya watumishi 290, wakiwemo maafisa sheria, maafisa urekebu na wasaidizi wa kisheria, wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutoa huduma hizo kwa ufanisi.
Aidha, matumizi ya mahakama mtandao yameendelea kurahisisha usikilizaji wa mashauri ya wafungwa na mahabusu, ambapo vituo 84 vya magereza nchini vina vifaa vya kutoa huduma hiyo.
Takwimu zinaonesha kuwa kuanzia Januari Mosi hadi Septemba 30, 2026, jumla ya mashauri 2,809 yamesikilizwa kupitia mfumo huo.
Matumizi ya mahakama mtandao yamesaidia kupunguza gharama za kuwasafirisha wafungwa na mahabusu kwenda mahakamani, kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa usafirishaji na kurahisisha mashauri kusikilizwa kwa wakati.
Utekelezaji wa makubaliano hayo unatarajiwa kuimarisha zaidi upatikanaji wa huduma za kisheria magerezani, huku ufuatiliaji na tathmini za mara kwa mara zikitarajiwa kusaidia kubaini changamoto na kuhakikisha haki za wafungwa na mahabusu zinalindwa kwa kuzingatia sheria, utu na usawa.



