Watendaji wapewa mafunzo utawala bora Manyara

MANYARA; Wizara ya Katiba na Sheria imesema migogoro mbalimbali inaweza kupata suluhisho ikiwa viongozi na watendaji wa serikali za mitaa watatekeleza majukumu kwa kuzingatia misingi ya demokrasia, utawala bora, haki za binadamu.
Mkurugenzi wa Katiba na ufuatiliaji wa wizara hiyo, Jane Lyimo amesema kwamba mafunzo yatasaidia kukuza uelewa kuhusu utawala bora na uraia, pamoja na kuwezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kama watumishi wa umma.
Amesema hayo katika mafunzo ya elimu ya uraia na utawala bora kwa viongozi na watendaji wa serikali za mitaa katika Halmashauri za Wilaya na mji wa Babati mkoani Manyara.
”Lengo la mafunzo haya ni kuwafikia viongozi na watendaji wa serikali za mitaa katika Halmashauri za Babati Mji na Babati Vijijini, ili kudumisha utawala bora na uraia,” amesema Lyimo.
Amesema Mkoa wa Manyara una migogoro mbalimbali ya ardhi, ambayo inaweza kuepukika na kutatuliwa iwapo viongozi na watendaji wa serikali za mitaa watatumia ipasavyo mbinu za utatuzi wa migogoro.

Kwa mujibu wake, utatuzi wa migogoro hiyo utasaidia wananchi kuachana na migogoro ya mara kwa mara na badala yake kuelekeza nguvu zao katika shughuli za maendeleo.
Amesema mafunzo hayo yatawasaidia viongozi na watendaji hao kupata mbinu za kuimarisha ushirikiano katika utatuzi wa migogoro mbalimbali, huku wakizingatia na kuheshimu mipaka ya majukumu yao.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Sangara wilaya ya Babati Vijijini Huseni Rashidi amesema katika kusikiliza matatizo ya watu ni lazima kuwa muwazi na mtunza siri za watu.
Naye Kalisti Msami, Mtendaji wa kijiji cha Kiru amesisitiza katika eneo la bonde la Kiru kuna migogoro ya ardhi na ya kifamilia itaweza kutatuliwa kwa urahisi kupitia mbinu zilizotolewa.



