Wanafunzi Watanzania kuunganishwa fursa za ajira, biashara China

CHINA; Balozi wa Tanzania nchini China, Dk Suleiman Haji Suleiman, ameahidi kuwaunganisha wanafunzi Watanzania wanaosoma nchini humo na kampuni za China ili kuwawezesha kupata fursa za ajira na biashara, na kuwataka kutumia ujuzi wanaoupata kuchangia maendeleo ya taifa.

Balozi Suleiman alitoa wito huo mapema wiki hii Jijini Beijing, China, wakati wa hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wapya Watanzania waliofika nchini humo kwa ajili ya masomo.

Alisema Tanzania inahitaji wataalamu wenye ujuzi na maarifa yatakayosaidia kukabiliana na changamoto za maendeleo, hivyo wanafunzi wanapaswa kutumia vizuri fursa ya elimu wanayoipata China ili kuwa na mchango wenye tija wanaporejea nchini.

Balozi huyo alisisitiza kuwa wanafunzi wanapaswa kutambua na kuchangamkia fursa zinazopatikana nchini China, hususan katika sekta za ajira na biashara, akiahidi kushirikiana nao kuwaunganisha na kampuni za China kwa lengo la kufungua milango ya fursa hizo.

Alisema uhusiano uliopo kati ya Tanzania na China unaweza kuwa chachu ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali, ikiwemo elimu, uwekezaji, biashara na uhamishaji wa ujuzi, hivyo wanafunzi wanapaswa kujiandaa kutumia maarifa yao kuleta manufaa kwa nchi.

Aidha, Dk Suleiman aliwataka Watanzania wanaoishi nchini China kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano, huku akiwahimiza kuzingatia sheria na taratibu za nchi hiyo ili kuepuka matatizo yanayoweza kuathiri maisha yao na taswira ya Tanzania.

Alisisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kuwa balozi mwema wa nchi yake kwa kuzingatia maadili, kuheshimu utamaduni wa wenyeji na kujenga mahusiano mazuri na watu wa mataifa mengine.

Aliongeza kuwa tabia na mwenendo wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi vina nafasi muhimu katika kuimarisha taswira ya taifa na kukuza uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi wanazoishi.

Hafla hiyo iliwakutanisha Watanzania wanaoishi na kufanya kazi Beijing pamoja na wanafunzi Watanzania wanaosoma Beijing na Tianjin lengo lilikuwa kuwakaribisha wanafunzi wapya na kuwawezesha kuungana na Watanzania wengine wanaoishi nchini China.

Hafla hiyo iliandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini China kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanafunzi Watanzania Beijing na Tianjin na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali ikiwemo wawakilishi wa Kampuni ya China Railway Construction Engineering Group na Oriental Holdings, Jumuiya za Wanafunzi wa Afrika nchini China.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button