TAFFA yaidhinisha utekelezaji wa mfumo wa T-CAMS

DAR ES SALAAM: Wanachama wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) wameidhinisha utekelezaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Ada ya Chini ya Mawakala wa Forodha (T-CAMS), baada ya viongozi kuwapa ufafanuzi kuhusu namna mfumo huo utakavyofanya kazi.

Uamuzi huo umefikiwa katika mkutano mkuu maalum wa wanachama wa TAFFA uliofanyika Dar es Salaam, ambapo suala la utekelezaji wa mfumo huo lilikuwa miongoni mwa ajenda kuu.

Wanachama walipata fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni na kupata ufafanuzi kuhusu mfumo huo kabla ya kupiga kura ya kuunga mkono utekelezaji wake kupitia Kampuni ya Capital Pay International.

Baadhi ya wanachama walisema walikuwa na maswali kuhusu mfumo huo kutokana na taarifa tofauti walizokuwa wakizipata, lakini ufafanuzi uliotolewa na uongozi wa TAFFA uliwawezesha kuelewa wajibu wao na namna T-CAMS itakavyofanya kazi.

“Sisi tulitaka kufahamishwa wajibu wetu ni upi, maana tulikuwa tukisikia kila mmoja anaongea anachojua yeye. Sasa viongozi wametufafanulia vizuri juu ya mfumo huo na namna utakavyofanya kazi, ndiyo maana unaona kwa pamoja tumeukubali bila pingamizi lolote,” alisema mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya uwakala, Godwin.

Mjadala huo pia ulihusisha masuala ya fedha na gharama zinazohusiana na mfumo huo.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika mkutano, fedha za wanachama hazitakatwa kupitia T-CAMS, huku gharama za mfumo huo zikitenganishwa na Agency Fees.

Aidha, wanachama walipewa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizokuwa zikitaja uwepo wa makato ya asilimia 30, ambapo waliambiwa kuwa utaratibu huo si sehemu ya mfumo uliowasilishwa kwao.

Uamuzi huo unakuja wakati Serikali ikisisitiza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika shughuli za clearing and forwarding, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuongeza uwazi na udhibiti katika sekta hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Rais wa TAFFA, Edward Urio, alisema uongozi wa chama hicho unalenga kuhakikisha maslahi ya wanachama yanalindwa wakati wa utekelezaji wa mfumo huo.

Urio alisema TAFFA pia inapaswa kuhakikisha utekelezaji wa T-CAMS unazingatia matakwa ya kisheria yaliyowekwa na Serikali kupitia GN Na. 83 ya mwaka 2026, hususan kuhusu matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kuripoti na kutangaza ada za huduma za clearing and forwarding.

“Dhamira ya uongozi ni kulinda maslahi ya wanachama, kuhakikisha uwazi katika utekelezaji wa mfumo na kuzingatia matakwa ya kisheria,” alisema.

Alisema mfumo huo unalenga kuimarisha uwazi na uwajibikaji, pamoja na kuhakikisha viwango vya chini vya ada za huduma vinafuatwa na kampuni zinazotoa huduma za clearing and forwarding.

Kwa mtazamo wa TAFFA, utekelezaji wa mfumo huo pia unatarajiwa kusaidia sekta hiyo kuendeshwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na kutokuzingatia taratibu zilizowekwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button