Vipimo sahihi kuongeza ushindani wa viwanda

DODOMA: WAKALA wa Vipimo (WMA) utashirikiana na viwanda kuhakikisha malighafi zinazoingizwa viwandani na bidhaa zinazozalishwa zinakidhi vipimo sahihi, huku ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa na utoaji wa elimu kwa wajasiriamali vikitumika kusukuma utekelezaji wa sera mpya za maendeleo ya viwanda na biashara ndogo na za kati.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihula, alisema hayo jana jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Biashara Ndogo na za Kati ya mwaka 2003, Toleo la 2025, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.
Alisema katika kutekeleza Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda, WMA itashirikiana na wazalishaji kuhakikisha malighafi wanazopokea zinapimwa kwa usahihi kwa kutumia vifaa vilivyohakikiwa, ikiwemo mizani mikubwa ya kupimia magari, matanki ya kuhifadhia mafuta na pampu za kupimia mafuta yanayotumika viwandani.
Alisema baada ya uzalishaji, wakala huo utaendelea kukagua bidhaa zilizofungashwa ili kuhakikisha zinakuwa na uzito na ujazo unaolingana na kiasi kilichoainishwa kwenye vifungashio.
Pia, alisema WMA itahakikisha bidhaa zinazouzwa kwa vipimo vya urefu na unene zinakidhi vipimo vilivyowekwa ili kulinda ubora na ushindani wa bidhaa hizo katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
“Lengo kubwa ni kuzifanya bidhaa zinazozalishwa kwenye viwanda hivi kuwa washindani kwenye soko la kimataifa lakini pia kwenye soko letu la kikanda,” alisema.
Kuhusu Sera ya Maendeleo ya Biashara Ndogo na za Kati, Kihula alisema WMA itaendelea kutoa elimu kwa wajasiriamali kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo vilivyohakikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo.
Alisema wajasiriamali wanaotumia mizani, vipimo vya ujazo na vya urefu wanapaswa kuhakikisha vifaa hivyo vimehakikiwa ili vipimo vinavyotumika katika biashara zao viwe sahihi.



