TNCC yasisitiza uaminifu kuimarisha biashara

KIGOMA: CHEMBA ya Taifa ya Biashara (TNCC) mkoani Kigoma imewataka wafanyabiashara wa mkoa huo kuzingatia uaminifu na uadilifu wanapofanya biashara na raia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.
Meneja wa TNCC Mkoa wa Kigoma, Prosper Guga, amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma, akieleza kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wafanyabiashara wa DRC kuhusu changamoto ya uaminifu Kigoma.
Amesema suala hilo hivyo vinaweza kudhoofisha imani na kuathiri ushirikiano wa kibiashara baina ya wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.

Guga amesema wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia maadili, kutimiza makubaliano na kujenga uaminifu, kwa kuwa biashara za kuvuka mipaka zinahitaji mahusiano ya muda mrefu na kuaminiana.
Ameeleza kuwa TNCC imeingia makubaliano na Chemba ya Biashara ya DRC kwa lengo la kukuza biashara na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa nchi hizo.
Katika hatua nyingine, amesema TNCC imeanza kushughulikia malalamiko ya mfanyabiashara mmoja kutoka DRC aliyedai kutapeliwa zaidi ya Sh milioni 90 na mfanyabiashara wa Kigoma mwaka 2024.
Amesema kupitia ufuatiliaji uliofanywa na taasisi hiyo, mfanyabiashara anayedaiwa kuhusika na deni hilo ameanza kurejesha fedha hizo, ambapo hivi karibuni alilipa Sh milioni 20.

Kwa upande wake, mfanyabiashara kutoka DRC, Anne Shilwalwa Maombi, amesema alikuwa akishirikiana na mfanyabiashara mmoja wa Kigoma aliyekuwa akimletea unga wa ngano kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma, kisha yeye kuusafirisha kwenda DRC.
Amesema kutokana na ushirikiano huo, alimwamini mfanyabiashara huyo na kumpatia Sh milioni 90 mwaka 2024 ili awe wakala wao, lakini fedha hizo zilitumika kwa manufaa yake binafsi badala ya kutekeleza makubaliano yao.



