Ushirikiano Tanzania, Japan wagusa sekta muhimu

DAR ES SALAAM: USHIRIKIANO kati ya Tanzania na Japan kupitia wataalamu wa kujitolea umeleta tija katika sekta tano ikiwemo elimu, afya, kilimo, uhandisi na maendeleo ya jamii kwa kusaidia kuhamisha ujuzi na utaalamu pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 60 ya programu hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alisema ushirikiano huo umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa.

Alisema katika kipindi cha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Programu ya Wajitolea wa Ushirikiano wa Nje wa Japan (JOCV), zaidi ya raia 1,700 wa Japan wamejitolea kufanya kazi nchini, wakiwemo walimu, madaktari na wahandisi.

Alisema wajitolea hao wamekuwa wakihudumu katika shule, hospitali, maeneo ya miradi na jamii mbalimbali, hususan maeneo yenye upungufu wa wataalamu na maeneo ya pembezoni.

Alisema katika sekta tajwa kila moja imepata ufanisi kwa kuwa wajitolea hao wameacha ujuzi na kuongeza tija hasa kwenye maeneo yaliyokuwa na uhaba wa wataalam hao, hivyo uwepo wao nchini una tija kubwa ya manufaa.

Alisema mbali na mchango wa wataalamu hao, Tanzania imenufaika na ushirikiano wa maendeleo kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), ikiwemo kupata mikopo ya masharti nafuu inayozidi Yen bilioni 147.3 (sawa na sh trilioni 2.46) na ruzuku inayozidi Yen bilioni 176.76 (sawa na sh trilioni 2.96).

“Zaidi ya Watanzania 22,000 wamenufaika na misaada ya kiufundi kupitia mafunzo yaliyotolewa nchini na Japan, huku serikali ikitarajia kuimarisha zaidi ushirikiano huo katika sekta za usafirishaji, nishati, maji, kilimo, afya na elimu,”alisema Mwandumbya.

Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini, Yoichi Mikami, alisema programu hiyo imeimarisha uhusiano wa watu wa mataifa hayo mawili, huku baadhi ya wajitolea waliofanya kazi Tanzania wakiendelea kukuza urafiki huo hata baada ya kurejea nchini kwao.

Alitoa mfano wa mmoja wa wajitolea aliyerejea Japan na kuchangia kuanzishwa kwa uhusiano wa miji pacha kati ya Nagai, katika Mkoa wa Yamagata nchini Japan na Dodoma.

Alisema wajitolea hao hawatoi ujuzi pekee, bali pia hujifunza kutoka kwa Watanzania na kujenga mahusiano ya kudumu na jamii wanazohudumia.

Naye Makamu wa Rais wa JICA, Hiroyuki Kobayashi, alisema programu hiyo itaendelea kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu na uhusiano kati ya Tanzania na Japan, akieleza kuwa mchango wake unaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Alisema ushirikiano huo haujajikita katika miradi ya miundombinu pekee, bali pia katika kuimarisha uwezo wa watu na maendeleo ya kijamii.

Akizungumzia mchango wa programu hiyo katika Dira ya 2050, Mwakilishi Mkazi wa JICA nchini, Dk Kuge Katsuya, alisema wajitolea 757 wametumwa katika maeneo yanayochangia vipaumbele vya dira hiyo, yakiwemo sayansi, hisabati, elimu na teknolojia ya kompyuta.

Alisema wajitolea hao pia wamechangia katika sekta za elimu, kilimo, ukunga na michezo kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa na jamii.

Alisisitiza kuwa kufikia malengo ya Dira ya 2050 kunahitaji uwekezaji katika rasilimali watu pamoja na mitaji, akieleza kuwa wataalamu wenye ujuzi ni muhimu katika kuleta mabadiliko ya uchumi.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Richard Kayombo, akizungumza kwa niaba ya makatibu tawala wa mikoa yote nchini, aliishukuru Serikali ya Japan kupitia JICA kwa mchango wake katika sekta za elimu, afya na miundombinu.

Alisema wananchi wamepata fursa ya kujifunza lugha, maarifa na mbinu mbalimbali kupitia kuishi na kufanya kazi pamoja na wajitolea hao, akihimiza ushirikiano huo kuendelea ili wananchi wengi zaidi wanufaike.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button