Kigoma Ujiji waja na mkakati kuondoa vyoo vya shimo

KIGOMA; Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, imetangaza mpango wa ujenzi wa vyoo bora katika shule za msingi na maeneo ya umma, ikiwa ni kuondoa vyoo vya shimo katika manispaa hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mansipaa ya Kigoma Ujiji, Juma Hamsini alisema hayo katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani ikiwa ni kikao chake cha kwanza tangu ateuilwe kuwa mkurugenzi wa manispaa hiyo na kubainisha kuwa wilaya hiyo kwa sasa ni ya mjini hivyo haina maana kwa shule za manispaa hiyo kuwa na vyoo vya shimo.

Amesema anakusudia kuwepo kwa vyoo bora katika maeneo yote ya umma, ili watu waweze kujisitiri badala ya kwenda kutafuta huduma hiyo kwenye mabaa na kuomba madiwani kumuunga mkono katika kutekeleza mipango hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mussa Maulid amemkaribisha rasmi mkurugenzi huyo na kuahidi kwa niaba ya madiwani kushirikiana naye kwa karibu katika kuibua, kutekeleza miradi na kusimamia mapato na matumizi ya halmashauri hiyo kwa manufaa ya wananchi.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Kigoma Mjini, Sadick Kaduro alimkaribisha mkurugenzi huyo katika halmashauri hiyo na kumweleza kuwa viongozi na wananchi wanapenda kupata maelezo na ufafanuzi wa mambo mbalimbali wanayotaka kusikia, hivyo asiogope kuulizwa na badala yake ajitahidi kutafuta majibu kwa mambo yote ambayo viongozi na wananchi wanataka kujua.



