MABADILIKO YA BOOST: Bil 604/- zajenga shule mpya 676 nchi nzima

MWANZA: SERIKALI imetumia Sh bilioni 604.66 kujenga shule mpya za msingi 676 kwa lengo la kuboresha mazingira ya wanafunzi kujifunza kwenye shule za msingi katika kipindi cha miaka minne.

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk Festo Dugange, alipokagua mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) katika Shule ya Msingi Isamilo, wilayani Sengerema mkoani Mwanza, jana.

Alisema kati ya shule 676 ambazo ni mpya shule 185 zimejengwa ndani ya maeneo ya shule za sekondari.
Alisema pia madarasa 16,822 yamejengwa ikiwamo madarasa 13,384 ya shule ya msingi na 3,438 ya awali sambamba na matundu ya vyoo 34,464 .
Aidha, Dk Dugange alisema mradi huo umewezesha kuongeza ufaulu kwa wanafunzi shule za msingi na kuboresha mazingira ya ufundishaji na kujifunza kwa shule za awali.

“Kwa mapenzi makubwa ya serikali yetu ya awamu ya sita inayooongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, zililetwa fedha hapa (Shule ya Msingi Isamilo) takriban shilingi milioni 541 zikajenga madarasa zaidi ya 14.

“Watoto wetu 1,336 wanasoma kwenye shule nzuri, shule bora, shule ya msingi Isamilo. Kama ambavyo siku zote serikali imekuwa ikisema, inawajali watoto wetu kwa kujenga shule bora kuhakikisha watoto wanasoma kwenye mazingira mazuri.”

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Issack Ramadhan, alisema mradi huo umesaidia kupunguza mrundikano wa wanafunzi darasani na kuondoa usumbufu wa wanafunzi kutembea umbali mrefu.

“Mradi umepunguza utoro wa wanafunzi, umesaidia kutoa elimu jumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, kupata ujuzi na maarifa mengi kwa kupitia vipindi vya MEWAKA na tumeimarisha mahusiano mema ya jamii inayozunguka shule, kuongezeka ufaulu wa wanafunzi na uandikishaji.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button