Tanzania mwenyeji maonesho ya Jua Kali 2027

KIGALI, RWANDA: Tanzania imechukua rasmi jukumu la kuwa mwenyeji wa Maonesho ya 27 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), maarufu kama Jua Kali, yanayotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2027.
Uteuzi huo unaipa Tanzania fursa muhimu ya kuonesha uwezo wa wajasiriamali wake, kukuza biashara na uwekezaji pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufuatia uteuzi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Alana Nchimbi, alisema Serikali ipo tayari kuhakikisha maandalizi na uratibu wa maonesho hayo yanafanyika kwa mafanikio makubwa.
Nchimbi alisema Tanzania imepokea jukumu hilo kwa furaha na kulichukulia kama heshima kubwa, huku ikitambua umuhimu wa maonesho hayo katika kukuza sekta ya wajasiriamali wadogo na wa kati.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunapokea kwa unyenyekevu na furaha kubwa nafasi hii ya kuwa nchi mwenyeji wa Maonesho ya 27 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.”
Aidha, ametoa shukrani kwa Sekretarieti ya EAC pamoja na nchi wanachama kwa kuonesha imani kwa Tanzania na kuipa heshima ya kuandaa tukio hilo muhimu la kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisisitiza kuwa Serikali itashirikiana kwa karibu na Sekretarieti ya EAC, serikali za nchi wanachama, sekta binafsi na wadau wengine kuhakikisha maandalizi yanafanyika kwa viwango vinavyostahili.
Alisema lengo ni kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa ya kihistoria, yanatoa fursa pana za kibiashara na kuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa wajasiriamali na wadau wote watakaoshiriki.
Maonesho ya Jua Kali ni jukwaa muhimu linalowaunganisha wajasiriamali wadogo na wa kati kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kuonesha bidhaa, kubadilishana uzoefu, kutafuta masoko na kujenga mitandao ya kibiashara.
Uenyeji wa Tanzania mwaka 2027 unatarajiwa kuongeza fursa za wajasiriamali wa ndani kutangaza ubunifu, bidhaa na huduma zao katika soko la kikanda na kuchochea ukuaji wa biashara baina ya nchi wanachama.



