NCMC yavutia uwekezaji biashara ya kaboni

UTURUKI:KITUO cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kimeihakikishia Kampuni ya Carbon Bridge ushirikiano wa kitaalamu katika uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya biashara ya kaboni nchini Tanzania, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuvutia wawekezaji wa kimataifa katika sekta hiyo.

Ahadi hiyo imetolewa wakati wa mazungumzo kati ya wataalamu wa NCMC na wawakilishi wa Carbon Bridge yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) jijini Antalya, Uturuki.

Katika mazungumzo hayo, Carbon Bridge imeeleza kuvutiwa na fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania, hususan katika miradi yenye uwezo wa kuzalisha viwango vya kaboni (Carbon Credits), ikitaja mazingira rafiki ya uwekezaji na mfumo wa usimamizi wa sekta hiyo unaoratibiwa na Serikali kupitia NCMC.

Kwa upande wake, NCMC imeeleza utayari wa kutoa ushirikiano wa kitaalamu na kuhakikisha uwekezaji huo unazingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali. Aidha, imeeleza kuwa kampuni hiyo tayari imewekeza katika miradi ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo matumizi ya majiko yaliyoboreshwa.

Tanzania inaendelea kufungua fursa za uwekezaji wa biashara ya kaboni katika sekta za misitu, kilimo, nishati, maji na usimamizi wa taka, ambazo zina uwezo wa kuongeza kipato cha jamii na kuchochea maendeleo endelevu.

Katika mkutano huo, NCMC iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji, Usajili na Utoaji Taarifa za Miradi, Dk. Deo Shirima; Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Mazingira, Ushauri na Utafiti, Dk. Paul Lyimo; Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Risper Koyi; pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Ibrahim Hamidu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button