Serikali kudhibiti leseni za biashara kwa wageni

DAR ES SALAAM: Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Rajab Salum, ameitaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuimarisha usimamizi wa utoaji wa leseni za biashara kundi A ili kuhakikisha fursa zilizotengwa kwa Watanzania zinalindwa.
Salum ametoa maelekezo hayo Novemba 12, 2026, jijini Dar es Salaam, alipotembelea ofisi za BRELA na kufanya mazungumzo na menejimenti pamoja na watumishi wa taasisi hiyo.
Amesema BRELA inapaswa kuhakikisha wageni hawapati leseni za biashara kundi A zinazohusu shughuli zilizozuiliwa kwa wasio raia wa Tanzania kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 487A la mwaka 2025.
Aidha, ameelekeza leseni zilizotolewa kwa wageni kabla ya kuanza kutumika kwa katazo hilo zisiendelee kuhuishwa baada ya muda wake kumalizika.
Katika hatua nyingine, Salum amewataka vijana wenye bunifu na bidhaa mpya kuzisajili na kupata ulinzi wa haki za miliki ubunifu ili waweze kuzitumia kibiashara na kunufaika na kazi zao. Pia amewahimiza wafanyabiashara wadogo kusajili shughuli zao ili ziweze kutambulika kisheria.
Ameielekeza BRELA kuandaa kliniki maalumu kwa wasanii itakayowasaidia kusajili na kulinda bunifu zao, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza wizi wa kazi za ubunifu na migogoro inayoweza kujitokeza.
Vilevile, amezitaka kampuni zinazokabiliwa na changamoto za kiutendaji, hususan migogoro ya umiliki wa hisa, kutembelea ofisi za BRELA ili kupata msaada wa kitaalamu katika kutafuta suluhu.
Akitoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 wakala huo ulisajili kampuni 5,811, majina ya biashara 11,044 na kutoa leseni za biashara kundi A 8,171.
Amesema katika kipindi hicho BRELA pia ilisajili vyeti vya viwanda tisa na kutoa leseni za viwanda 283, huku ikisajili alama za biashara na huduma 1,075.
Nyaisa ameongeza kuwa wakala huo ulipokea maombi 95 ya hataza, akieleza kuwa takwimu hizo zinaonesha mwendelezo wa utoaji wa huduma za usajili na leseni kwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini.



