Bodaboda wajengewa uwezo kuokoa maisha

DAR ES SALAAM: Mafunzo ya usalama barabarani na huduma ya kwanza yaliyotolewa kwa waendesha pikipiki 1,624 jijini Dar es Salaam yanatarajiwa kuongeza uwezo wa kundi hilo kujilinda, kusaidia waathirika wa ajali na kuokoa maisha wakati wa dharura.
Mafunzo hayo yametolewa na Kampuni ya Tanzania Breweries PLC (TBL) kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS), kupitia programu iliyoanza mwaka 2024 kwa lengo la kuwajengea waendesha pikipiki maarifa ya usalama na stadi za kukabiliana na dharura.
Idadi ya waliofikiwa imevuka lengo la awali la watu 1,600 na kufikia asilimia 102, kupitia mafunzo yaliyofanyika katika wilaya zote tano za Dar es Salaam.
Katika mafunzo hayo, waendesha pikipiki wamejifunza matumizi sahihi ya helmeti, sheria na kanuni za barabarani, uendeshaji wa tahadhari, ufanyaji maamuzi salama na hatua za kuchukua mtu anapokutana na tukio la dharura.
Umuhimu wa mafunzo hayo unatokana na nafasi ya waendesha pikipiki katika shughuli za kila siku za jamii, ikiwemo kusafirisha abiria, bidhaa na kuunganisha maeneo mbalimbali. Kutokana na shughuli zao, mara nyingi huwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika katika maeneo ya ajali na wanaweza kutoa msaada wa awali kabla ya wahudumu wa afya kufika.
Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria na Uhusiano wa Kampuni wa TBL, Neema Temba, amesema usalama barabarani unahusu zaidi ya kuzuia ajali, kwa kuwa unalinda maisha ya watu, familia zao na vyanzo vyao vya kipato.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania, Lucia Pande, amesema elimu ya huduma ya kwanza inawawezesha waendesha pikipiki kuwa sehemu ya suluhisho wakati wa dharura, huku akisisitiza kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja.
Pamoja na mafunzo hayo, TBL imehimiza waendesha pikipiki na watumiaji wengine wa barabara kuepuka kuendesha vyombo vya moto baada ya kunywa pombe, ikisisitiza umuhimu wa kufanya maamuzi yanayolinda maisha.
Kwa ujumla, mpango huo unaweka mkazo katika kujenga utamaduni wa tahadhari, uwajibikaji na kusaidiana katika jamii, ili kupunguza madhara ya ajali na kuongeza usalama kwa watumiaji wote wa barabara.



