Jamii yahimizwa mazoezi kuepuka magonjwa

DAR ES SALAAM: Jamii imetakiwa kuzingatia mazoezi ya mwili, ulaji wa chakula bora na mabadiliko chanya ya mtindo wa maisha ili kupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari, ambao ni miongoni mwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Wito huo umetolewa na Chama cha Wagonjwa wa Kisukari Tanzania katika maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani yanayofanyika Novemba 14 kila mwaka, huku kikisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii ili kuchukua hatua za mapema kujikinga na ugonjwa huo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Meneja Mradi wa Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza kutoka chama hicho, Dk. Rachel Mungu, amesema kufanya mazoezi mara kwa mara ni njia muhimu ya kupunguza hatari ya kupata kisukari.

Ameshauri jamii kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki kwa muda wa dakika 30, pamoja na kushiriki shughuli mbalimbali zinazosaidia kuufanya mwili kuwa katika hali ya uchangamfu.
Dk. Rachel amesema mabadiliko ya mtindo wa maisha, ikiwemo kupungua kwa shughuli za kimwili kutokana na maendeleo ya teknolojia na ongezeko la matumizi ya vyombo vya usafiri, yamechangia watu wengi kutofanya mazoezi ya kutosha.
Aidha, amebainisha kuwa ulaji usiozingatia mlo kamili, hususan matumizi ya vyakula vyenye wanga kwa wingi bila kujumuisha mboga za majani, matunda na makundi mengine ya vyakula, unaweza kuongeza hatari ya kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Watoto na Magonjwa ya Homoni kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Monica Appollo, amesema takribani asilimia 90 ya watoto wanaogundulika kuwa na kisukari hufikishwa hospitalini katika hali mbaya na kuhitaji kulazwa, jambo linaloonesha changamoto ya uelewa kuhusu ugonjwa huo katika jamii.
Amesisitiza umuhimu wa kuongeza elimu kuhusu dalili za kisukari kwa watoto ili wazazi na walezi waweze kutambua mapema viashiria vya ugonjwa huo na kuwafikisha watoto hospitalini kwa uchunguzi na matibabu.



