Kampuni za bima zatakiwa kupata vyeti vya ISO

DODOMA: SERIKALI imezitaka kampuni za bima nchini kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ubora na kuchukua hatua za kupata cheti cha kimataifa cha ISO 9001:2015 ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na kuboresha huduma kwa wateja.

Wito huo umetolewa Novemba 18, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Natu El-Maamry Mwamba, wakati wa hafla ya makabidhiano ya cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), iliyofanyika Bima House, Njedengwa jijini Dodoma.

Amesema hatua ya TIRA kupata cheti hicho inaonesha dhamira ya taasisi hiyo katika kuimarisha mifumo ya kiutendaji, uwajibikaji na utoaji wa huduma kwa kuzingatia viwango vinavyotambulika kimataifa.

Ameeleza kuwa ubora wa huduma ni msingi wa kujenga imani ya wananchi na wadau katika sekta ya bima, hivyo ni muhimu kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati, uwazi na weledi, huku mifumo ya utendaji ikiendelea kuboreshwa ili kukidhi matarajio ya wateja.

Aidha, ameitaka TIRA kuhakikisha cheti hicho hakibaki kuwa nyaraka ya kutunzwa ofisini, bali kiwe msingi wa kujenga utamaduni wa kazi unaozingatia ubora katika kila jukumu.

Amewataka watumishi kuendelea kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utendaji katika kutekeleza majukumu yao.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Bima, Khadija I. Said, amesema mafanikio ya TIRA kupata cheti hicho yametokana na ushirikiano na juhudi za pamoja za watumishi katika kukamilisha mchakato huo.

Naye Kamishna wa Bima, Dk. Baghayo Saqware, amesema mchakato wa kupata cheti hicho ulianza rasmi Januari 2025, baada ya TIRA kuwasilisha maombi ya usajili kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Novemba 7, 2024.

Amesema baada ya maombi hayo, TIRA ilipata mwongozo pamoja na mpango kazi wa utekelezaji Desemba 11, 2024

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button