BoT yaimarisha ujumuishi wa kifedha kwa walemavu

IRINGA: Walemavu mkoani Iringa wameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kutoa elimu ya fedha inayowasaidia kuelewa utunzaji sahihi wa fedha, matumizi ya mikopo na namna ya kutambua alama za usalama zilizopo kwenye noti, huku wakiiomba benki hiyo kupanua wigo wa mafunzo hayo ili yawafikie walemavu wengi zaidi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini.

Pongezi hizo zimetolewa leo Alhamisi, Novemba 19, 2026, na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Mkoa wa Iringa, Shabani Shomari, wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyoandaliwa na BoT mkoani humo.

Shomari amesema elimu ya fedha ina umuhimu mkubwa kwa watu wenye ulemavu kwa kuwa inawawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

“Tunaishukuru BoT kwa kutupatia nafasi hii ya kupata elimu ambayo walemavu wanastahili kuipata, hasa katika kipindi ambacho nchi inaelekea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. Hata hivyo, tunatamani elimu hii iwafikie walemavu wengi zaidi, hasa wale wanaoishi vijijini,” amesema.

Awali, akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa huo, Ashery Mndalila, amewataka washiriki kutumia elimu waliyoipata kuwa mabalozi katika jamii kwa kuhamasisha utunzaji bora wa fedha, matumizi sahihi ya mikopo na utambuzi wa alama za usalama kwenye noti.

Kwa upande wake, Ofisa wa Benki Kuu, Sadi Makomba, amesema BoT itaendelea kutoa elimu hiyo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya fedha na uchumi.

BoT inaendelea kutekeleza programu za elimu ya fedha na uchumi kwa makundi mbalimbali ya jamii, yakiwemo watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufanikisha azma ya ujumuishi wa huduma za fedha kwa asilimia 100.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button