Tanzania yalenga kuvutia wawekezaji viwanda vya madini

DAR ES SALAAM: TANZANIA imejipanga kuvutia wawekezaji zaidi wa ndani na nje ya nchi kuanzisha viwanda vya uchakataji na uongezaji thamani wa madini, kwa kuweka mazingira wezeshi yanayojumuisha maeneo maalum ya uwekezaji, upatikanaji wa nishati ya uhakika, miundombinu ya usafirishaji na unafuu wa kikodi.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Serikali ina dhamira ya kuifanya Tanzania kuwa kituo muhimu cha uwekezaji katika shughuli za kuongeza thamani ya madini, huku ikiwakaribisha wawekezaji kutumia fursa zilizopo nchini kuanzisha viwanda na kushiriki katika kukuza uchumi.

Akizungumza Novemba 21, 2026, wakati wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji (TMIC 2026), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Mavunde amesema Serikali imeweka mazingira yanayolenga kupunguza vikwazo vya uwekezaji na kuhakikisha wawekezaji wanapata mahitaji muhimu ya kuendesha viwanda vya madini.

Amesema eneo la ekari 1,331 katika eneo la mgodi wa zamani wa Buzwagi, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, limetengwa na kugeuzwa kuwa Eneo Maalum la Kiuchumi la Buzwagi (Buzwagi Special Economic Zone), kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kuanzisha viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani ya madini.

Ameeleza kuwa Serikali pia inawekeza katika upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa kuwa viwanda vya kuyeyusha na kuchakata madini vinahitaji umeme mwingi ili kuendesha shughuli zake.

Kwa mujibu wa Mavunde, Serikali inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, hatua inayotarajiwa kusaidia mahitaji ya viwanda na kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda.

ALSO READ: Serikali yaweka mikakati kuongeza thamani ya madini

Katika eneo la miundombinu, amesema Serikali inaendelea kuboresha bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza uwezo wa kupokea meli na kuhudumia mizigo mingi kwa wakati mmoja.

Pia amesema ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR unaendelea kuimarisha muunganiko wa maeneo mbalimbali nchini, huku akieleza kuwa reli hiyo inatarajiwa kuunganisha Tanzania na Musongati nchini Burundi, eneo lenye shughuli za uchimbaji wa madini ya nikeli.

Ameongeza kuwa reli ya TAZARA nayo ni sehemu ya miundombinu ambayo itatumika kusaidia usafirishaji wa madini na bidhaa zitakazochakatwa nchini.

Aidha, Mavunde amesema Serikali inaendelea kupanua wigo wa utafiti wa madini ili kuhakikisha uwepo wa malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda vitakavyoanzishwa na wawekezaji.

Amesema uhakika wa malighafi ni miongoni mwa mambo muhimu yanayozingatiwa na wawekezaji kabla ya kuamua kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya madini katika nchi husika.

Ameeleza kuwa hatua hizo zinaenda sambamba na sera na sheria zinazohimiza uchakataji wa madini nchini kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

Akizungumzia mchango wa sekta hiyo katika uchumi, Mavunde amesema madini yanachangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa, hali inayoonesha umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi na kuongeza fursa za uwekezaji.

Amewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo kuwekeza Tanzania, akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kisera, kisheria, kifedha na katika miundombinu pamoja na kutoa unafuu wa kikodi ili kuwezesha uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani ya madini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button