Kutoka kuwa muuguzi hadi kupamba marehemu
DAR ES SALAAM: ‘UOGA WAKO NDIO UMASIKINI WAKO’, Hivi ndivyo tunaweza kusema, wakati watu wengi wakihusisha kazi ya urembo na watu walio hai, Eva Hillary Mbuya, mwenye umri wa miaka 44, ameamua kuvunja mtazamo huo kwa kutumia ujuzi wake wa upambaji kuwahudumia watu ambao tayari wamefariki dunia.
Kupitia kampuni yake ya Sacred Touch Artistry, Eva ameingia katika eneo ambalo bado ni geni kwa sehemu kubwa ya jamii ya Tanzania, akijikita katika huduma ya kupamba na kurejesha mwonekano wa miili ya marehemu kabla ya kuagwa na ndugu, jamaa na marafiki.
Kwa Eva, huduma hiyo si suala la urembo pekee, bali ni namna ya kumheshimisha marehemu, kulinda utu wake na kuwasaidia wafiwa kubaki na kumbukumbu nzuri za mwisho za wapendwa wao.
Akizungumza na Daily News Digital, Eva anasema wazo la kuanzisha huduma hiyo lilitokana na kutambua kuwa licha ya kuwa na ujuzi wa upambaji, kulikuwa na kundi ambalo halikuwa likipata huduma hiyo, nalo ni watu waliopoteza maisha.
Eva anasema aliona fursa ya kutumia ujuzi wake katika eneo ambalo lilikuwa na uhitaji lakini halijapewa kipaumbele, tofauti na huduma za kawaida za urembo zinazolenga watu walio hai.
“Sababu pekee iliyonifanya nifikirie kupamba marehemu ni kwamba niliona wao ndio ambao bado hawana huduma. Kwa ujuzi wa makeup niliokuwa nao, niliona sehemu pekee ambayo ningeweza kuutumia na ambayo bado inahitaji huduma ni kwao,” anasema.
Urembo kwa marehemu ni heshima
Eva anaeleza kuwa mwili wa binadamu hupitia mabadiliko baada ya kifo, hali inayoweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa mwonekano wa marehemu, hasa pale kifo kinapotokana na ajali au ugonjwa uliosababisha mwili kuathirika.
Kwa mujibu wake, mabadiliko hayo yanaweza kufanya ndugu washindwe kumtambua marehemu kama walivyomzoea alipokuwa hai, jambo linaloweza kuongeza maumivu ya kihisia wakati wa kuaga.
Anasema huduma ya urembo wa marehemu inalenga kurejesha mwonekano unaowezekana ili familia iweze kumuaga mpendwa wao katika hali yenye utulivu na heshima.
Anataja sababu tatu kuu zinazomfanya aone umuhimu wa huduma hiyo: kurejesha mwonekano wa marehemu kadiri inavyowezekana, kumtunza na kumpa heshima anayostahili, na kuwapa wafiwa kumbukumbu nzuri za mwisho.
“Unapomwangalia marehemu kwa mara ya mwisho, unapaswa kubaki na picha nzuri ya mtu uliyemfahamu, badala ya kukumbuka mwonekano uliobadilika kiasi cha kukutisha. Tunataka ndugu waweze kumuaga bila kuongeza maumivu mengine ya kihisia,” amesema Eva.
Uzoefu wa uuguzi umemjengea ujasiri kuhudumia marehemu
Ingawa kazi hiyo inaweza kuonekana kuwa ngumu kwa watu wengi, hasa kutokana na hofu inayohusishwa na miili ya marehemu, Eva anasema kwake si jambo geni.
Hii inatokana na historia yake ya kitaaluma katika sekta ya afya. Alisoma Shule ya Sekondari ya Msalato na baadaye Jangwani High School kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Muhimbili, ambako alipata Shahada ya Sayansi ya Uuguzi (Bachelor of Science in Nursing).
Pia ana Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Uuguzi, akibobea katika huduma za wagonjwa mahututi na majeraha makubwa (Critical Care and Trauma).
Anasema uzoefu wake wa kuhudumia wagonjwa mahututi na wa ajali, wakiwemo baadhi waliofariki wakati wakipatiwa matibabu, ulimsaidia kujenga uwezo wa kufanya kazi katika mazingira yanayoweza kuwa magumu kihisia na kimwili.
“Ujasiri huo nimeujenga kwa muda mrefu. Nimekuwa nikiona watu wakifariki mikononi mwangu wakati nikiwa katika majukumu ya kuwahudumia. Kwa hiyo, tayari nilikuwa nimezoea mazingira hayo kupitia mafunzo na vitendo,” anasema.
Imani potofu ndio changamoto kubwa
Pamoja na kuwa na ujasiri na uzoefu unaomsaidia kutekeleza majukumu yake, Eva anakiri kuwa changamoto kubwa aliyokutana nayo tangu alipoanzisha huduma hiyo ni uelewa mdogo wa jamii.
Anasema alipoanza kuitangaza rasmi Sacred Touch Artistry, aligundua kuwa watu wengi hawakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu umuhimu wa kupamba marehemu, huku wengine wakiwa na mitazamo na imani potofu kuhusu huduma hiyo.
Hali hiyo imemfanya abadili kwa kiasi fulani namna anavyoendesha biashara yake, kwa kuweka mkazo mkubwa katika kutoa elimu kwa jamii kabla ya kutarajia huduma hiyo kukubalika kwa upana.
Anasema maoni na mijadala iliyojitokeza kwenye mitandao ya kijamii baada ya kujitangaza haikumkatisha tamaa, bali ilimsaidia kutambua kiwango cha uelewa wa jamii na maeneo yanayohitaji elimu zaidi.
“Nilipoanza nilikuwa na lengo la kujitambulisha na kuongeza uelewa. Nilipoyaona maoni ya watu, niligundua kuwa wengi hawana uelewa wa kutosha. Kwa hiyo, kwangu yalikuwa tathmini ya namna ninavyopaswa kuongeza nguvu katika kutoa elimu,” anasema.
Anaongeza kuwa familia yake, wakiwemo watoto wake wanne na ndugu zake, imekuwa ikimuunga mkono katika shughuli hiyo. Anasema watoto wake wamezoea mazingira ya kazi zake za awali katika sekta ya afya, hivyo hawajaona huduma hiyo kama jambo geni.
Kila marehemu ana mahitaji yake
Katika kutekeleza huduma hiyo, Eva anasema jambo la msingi ni kuwasikiliza ndugu wa marehemu kabla ya kuanza kazi.
Anasema kwa kuwa hamfahamu marehemu alivyoishi, alivyopenda kuonekana au imani zake, ni muhimu kuzungumza na familia ili kufahamu aina ya mwonekano wanaoutaka.
Kwa kufanya hivyo, huduma inayotolewa inazingatia matakwa ya familia badala ya kutumia mtindo mmoja wa urembo kwa kila marehemu.
Pia, anasema huchukua picha za kabla na baada ya huduma kwa ajili ya kumbukumbu na kuwasaidia ndugu kuelewa mabadiliko yaliyofanyika, hasa pale mwili unapokuwa tayari umeathirika kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo, anakiri kuwa si kila mwili unaweza kurejeshewa mwonekano unaotakiwa. Baadhi ya miili inayopokelewa huwa imeharibika sana kutokana na ajali au mabadiliko yanayotokea baada ya kifo.
Katika mazingira hayo, anasema wakati mwingine kazi huwa ngumu na huhitaji muda zaidi, huku akisisitiza kuwa kuna hali ambazo haziwezi kurekebishwa kwa kutumia vipodozi pekee.
Anasema endapo mwili umeharibika kiasi ambacho hauwezi kushughulikiwa kwa usalama na kufikia matokeo yanayotarajiwa, familia hushauriwa kuuchukua utaratibu wa kuufunika badala ya kuuonyesha.
Kumhudumia marehemu bila kudhalilisha utu wake
Jambo jingine analolipa kipaumbele ni kutenganisha masuala ya malipo na utekelezaji wa huduma.
Eva anasema makubaliano ya kifedha hufanyika kabla ya kuanza kazi ili kuepusha hali ya ndugu kuanza kutafuta fedha wakati huduma inaendelea au watu wakiwa wanasubiri marehemu kuagwa.
Kwa mtazamo wake, hali hiyo inaweza kumdhalilisha marehemu na kuathiri heshima inayopaswa kuzingatiwa wakati wa kutoa huduma.
Anasisitiza kuwa anapokuwa akifanya kazi, hamchukulii marehemu kama mteja wa kawaida, bali kama binadamu anayehitaji huduma, huku mteja wake akiwa ni ndugu au familia iliyomtafuta.
Hata hivyo, anakiri kuwa changamoto nyingine ni muda wa maandalizi, hasa kwa kuwa kwa sasa hana ofisi maalumu na hutegemea eneo linaloandaliwa na familia ya marehemu.
Anasema baadhi ya familia hushindwa kuelewa muda unaohitajika kufanya maandalizi hayo, jambo linaloweza kuleta shinikizo wakati ndugu na jamaa wakiwa wanasubiri kuaga.
Anakumbuka kuwa katika kazi yake ya kwanza, aliyofanya kwa kujitolea, alikutana na changamoto ya muda baada ya familia kutambua kuwa huduma ya makeup inaweza kukamilika ndani ya dakika chache. Hali hiyo ilimlazimu kufanya maandalizi kwa haraka baada ya ratiba ya kuaga kusogea.
Tangu wakati huo, anasema amejifunza umuhimu wa kuweka makubaliano ya muda kabla ya kuanza kazi.
Biashara changa yenye matarajio ya kukua
Licha ya kuanza biashara hiyo hivi karibuni, Eva anasema tayari amepata wateja, jambo analolichukulia kuwa mafanikio ya awali kutokana na ugeni wa huduma hiyo katika soko la Tanzania.
Anasema changamoto ya uelewa mdogo wa jamii ndiyo inayofanya biashara hiyo kutokua kwa kasi anayoitarajia, licha ya kuwepo kwa uhitaji unaoweza kujitokeza kutokana na vifo vinavyotokea kila siku.
Kwa sasa, amekuwa akipokea mawasiliano kutoka mikoani, yakiwemo ya watu wanaohitaji huduma hiyo na wasanii wa vipodozi wanaotaka kujiunga naye.
Anasema yuko tayari kutoa huduma nje ya Dar es Salaam na hata nje ya Tanzania, iwapo gharama za usafiri na malazi zitafanyiwa utaratibu.
Kwa mtazamo wa kibiashara, anaeleza kuwa uamuzi wake wa kuingia katika eneo hilo ulitokana pia na tathmini ya ushindani. Badala ya kuingia katika soko la urembo wa kawaida ambako wasanii wengi tayari wanatoa huduma, aliamua kujikita katika eneo ambalo aliona bado halijafanyiwa kazi kwa kiwango kikubwa.
Wito wa Eva kwa wenye ndoto
Mbali na kuzungumzia biashara yake, Eva anatoa ujumbe kwa wanawake ambao wana ndoto za kuanzisha shughuli mbalimbali lakini wanahofia umri, mitazamo ya jamii au kuchelewa kutimiza malengo yao.
Akitumia maisha yake kama mfano, anasema akiwa na umri wa miaka 44 na mama wa watoto wanne, bado ameona nafasi ya kuanza jambo jipya na kuchangia katika maendeleo ya jamii.
Anasema mafanikio hayapaswi kuwekewa ukomo wa umri, bali mtu anapaswa kujiamini na kufuatilia ndoto zake mradi shughuli anayokusudia kufanya ni halali na haiwaletei madhara wengine au mazingira.
“Usijali unaanzia wapi. Mimi nina miaka 44, ni mama wa watoto wanne, lakini bado niko hapa naanzisha kitu kipya. Maadamu bado unaishi, bado una nafasi ya kufanya jambo unalolitamani,” anasema.
Pia anatoa wito kwa Serikali kuongeza fursa za uwezeshaji, mafunzo na mentorship kwa wanawake wenye umri wa miaka 40 na kuendelea, akisema kundi hilo bado lina uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa lakini mara nyingi hukosa kupewa nafasi zinazolingana na uwezo wao.
Anasema licha ya kuwa na elimu ya uzamili, kuanza upya katika shughuli za kiuchumi na kitaaluma kunaweza kuwa changamoto kutokana na mifumo inayosisitiza uzoefu wa kazi na fursa ambazo wakati mwingine huwa hazizingatii hali ya wanawake waliotumia muda mwingi kulea familia.
Kwa Eva, kuanzisha Sacred Touch Artistry si mwanzo wa biashara pekee, bali pia ni safari ya kuonyesha kuwa ujuzi unaweza kutumika katika maeneo yasiyozoeleka, na kwamba heshima ya binadamu haipaswi kuishia anapofariki dunia.



