Wanafunzi 90 kusoma sayansi, teknolojia Algeria

BALOZI wa Tanzania nchini Algeria, Mobhare Matinyi, amewataka wanafunzi 90 waliokwenda nchini humo kupitia Programu ya Ufadhili wa Masomo ya Samia (Samia Scholarship) kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao na kuwa fahari ya Taifa.

Akizungumza na wanafunzi hao katika Chuo Kikuu cha Blida, kilichopo umbali wa kilomita 45 kutoka mji wa Algiers, Balozi Matinyi amewasisitiza kudumisha umoja na kuishi kwa mshikamano, akiwakumbusha kuwa wanabeba heshima ya Tanzania kupitia programu hiyo ya ufadhili.

“Tambueni kwamba mnaibeba heshima ya nchi yetu kupitia Samia Scholarship, ambayo ni alama ya heshima ya ubora kitaaluma,” amesema. Katika mazungumzo hayo, Balozi Matinyi aliambatana na viongozi wa Chuo Kikuu cha Blida pamoja na ujumbe wa Serikali kutoka Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Blida, Profesa Bachir Amer, amewasilisha salamu za Waziri wa Elimu ya Juu na Utafiti wa Kisayansi wa Algeria, Profesa Kamel Bidari, kwa Balozi Matinyi, ujumbe wa Serikali na wanafunzi hao.

Kiongozi wa ujumbe wa Serikali uliowasindikiza wanafunzi hao, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Elimu ya Juu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Steven Maluka amesema ni mara ya kwanza kwa Serikali kugharamia kundi kubwa la wanafunzi 90 kwenda nje ya nchi kusomea shahada za sayansi na teknolojia.

“Hii ni mara ya kwanza kwa Serikali ya Tanzania kugharamia kundi kubwa la wanafunzi bora 90 kwenda nje ya nchi kusomea shahada za sayansi na teknolojia,” amesema. SOMA: Kiingereza kuwa kigezo wanufaika Samia Scholarship

Profesa Maluka ameungana na Balozi Matinyi kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za ufadhili zilizowapa wanafunzi hao fursa ya kusomea fani za sayansi na teknolojia nchini Algeria.

Ujumbe wa Serikali uliowasindikiza wanafunzi hao pia ulijumuisha Afisa Mwandamizi wa Wizara hiyo, Dkt. Fabian Nyenyembe, na Mratibu wa Samia Scholarship, Profesa Liliane Pasape, kutoka Chuo Kikuu cha Afrika cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST), kilichopo Arusha.

Wanafunzi hao waliwasili nchini Algeria Novemba 24, 2026, kwa ndege ya Shirika la Ndege la Qatar na kupokelewa na Balozi Matinyi, maofisa wa Ubalozi pamoja na watendaji wa Wizara ya Elimu ya Juu na Utafiti wa Kisayansi ya Algeria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Houari Boumediene, jijini Algiers.

Wanafunzi hao wanatarajiwa kusomea fani za afya, sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Algeria, walikopangiwa kwa kuzingatia ufaulu wao wa kitaaluma nchini Tanzania.

Vyuo vikuu vilivyopokea wanafunzi hao ni Algiers, Annaba, Batna, Blida, Boumediene, Boumerdes, Chlef, Constantine, Mostaganem, Oran, Setif, Sidi Bel Abbes, Skikda na Tiaret. Mbali na masomo yao, wanafunzi hao wanatarajia kujifunza lugha za Kifaransa au Kiarabu ili kuwawezesha kuwasiliana na jamii ya nchini humo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button