Afrika yasisitizwa utafiti kutatua changamoto za wananchi

ARUSHA: MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Usimamizi wa Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI), Profesa Peter Kiruku, amezitaka nchi za Afrika kuongeza uwekezaji katika utafiti na ubunifu ili kuzalisha suluhisho zinazokidhi mahitaji ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika bara hilo.
Amesema Afrika inahitaji kujenga mifumo imara ya kufadhili tafiti, kutumia matokeo yake katika kutengeneza bidhaa na huduma, pamoja na kuhakikisha maarifa yanayozalishwa na wataalamu wa bara hilo yanatumika kuboresha maisha ya jamii.
Akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Utafiti la ESAMI lililofanyika kwa siku tatu jijini Arusha jana, Profesa Kiruku amesema Afrika inapaswa kuimarisha uwezo wake wa kuzalisha maarifa na teknolojia badala ya kutegemea kwa kiwango kikubwa mifumo na uvumbuzi kutoka nje ya bara hilo.
Amesema eneo la teknolojia ya Akili Unde (AI) linahitaji kuangaliwa kwa makini, akibainisha kuwa mifumo ya teknolojia hiyo inaweza kuwa na upendeleo unaotokana na mazingira ilikotengenezwa, hali inayoweza kuathiri namna Waafrika wanavyotafsiri na kutumia matokeo yake.
Ameeleza kuwa ni muhimu kwa watafiti na serikali za Afrika kuchunguza mifumo hiyo na kuhakikisha matumizi yake yanazingatia mazingira, mahitaji na vipaumbele vya bara hilo, badala ya kuyachukulia matokeo yake kuwa ukweli usiopingika.
Profesa Kiruku amesema pia kuna umuhimu wa kubadili namna mafanikio ya utafiti yanavyopimwa, akisisitiza kuwa thamani yake haipaswi kuishia katika machapisho ya kitaaluma, bali ionekane kupitia uwezo wa kutatua changamoto halisi za jamii.
Amesema matokeo ya tafiti yanapaswa kutumika kuboresha shughuli za kiuchumi, huduma za jamii na uzalishaji, huku yakisaidia taasisi za umma na sekta binafsi kufanya maamuzi yanayotokana na ushahidi.
Ameongeza kuwa biashara na matumizi ya matokeo ya utafiti ni sehemu muhimu ya kupima athari zake, kwani tafiti zinapogeuzwa kuwa bidhaa, huduma au suluhisho la changamoto za jamii, huwa na mchango mkubwa katika maendeleo.
Akizungumzia namna ya kufanikisha hilo, amependekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya vyuo vikuu, sekta ya viwanda, taasisi za sayansi na miliki bunifu, pamoja na taasisi za utafiti na ushauri wa sera.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuweka mifumo rasmi ya ushirikiano kati ya vyuo vikuu na viwanda katika kuhamisha teknolojia na maarifa ili matokeo ya tafiti yatumike katika vitendo badala ya kubaki kwenye makabrasha na maktaba.
Profesa Kiruku pia ameeleza umuhimu wa kuanzisha mifumo ya ufadhili wa pamoja wa tafiti za Afrika, akipendekeza ushirikiano wa benki za biashara, mabaraza ya utafiti na sera, washirika wa maendeleo pamoja na sekta ya viwanda.
Amesema mfumo huo wa ufadhili mseto wa utafiti unaomilikiwa na kuongozwa na Afrika (blended sovereign research financing) utasaidia kuongeza rasilimali za tafiti na kuhakikisha matokeo yake yanatumika.
Katika kongamano hilo lililofanyika kwa siku tatu, washiriki walijadili kupitia vikao 41 maeneo mbalimbali ya utafiti, ushirikiano wa kimkakati, miundombinu ya kisasa ya utafiti, matumizi ya teknolojia ya Akili Unde na namna ya kugeuza matokeo ya tafiti kuwa suluhisho la kiuchumi na kijamii.



