Watoto 60 kutibiwa bure moyo BMH
WATOTO 60 wenye umri usiozidi miaka 14 wenye matatizo ya moyo watapata matibabu ya bure katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kuanzia mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, Dk Alphonce Chandika, amesema kuwa hopitali rafiki ya BMH ya Sri Sathya Sai Sanjeevan ya India wamekubali kugharamia matibabu kwa watoto 60 wenye matatizo ya moyo kupata matibabu BMH.
“Tunaenda kuingia makubaliano ya ushirikiano (MOU) na Hospitali ya Sri Sathya Sai Sanjeevan ya India,” amesema wakati akitoa taarifa ya ziara yake ya Kigali, Rwanda ambako alikutana na viongozi wa hospitali hiyo inayoongoza kwa matibabu ya moyo India.

Dk Chandika amesema ushirikiano kati ya BMH na hospitali hiyo ya India utasaidia pia kuimarisha huduma za matibabu ya moyo BMH.
“Pia Hospitali ya Sri Sathya Sanjeevan pia watagharamia mafunzo kwa wataalamu 15 wa moyo wa BMH nchini India,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Hospitali, Jeremiah Mbwambo, ameishukuru Hospitali ya Sri Sathya Sanjeevan ya India kwa msaada huu.
“Kuwahudumia bure watoto 60 wenye matatizo ya moyo kila mwaka ni kuonesha shukrani kwa jamii tunayoihudumia. Tunarudisha kwa jamii,” alisema.



