Serikali kuangalia uwezekano wa internet maeneo ya umma

SERIKALI imesema itaendelea kuangalia uwezekano wa kufunga mtandao wa ‘Wifi ‘kwa ajili ya huduma ya ‘Internet’ katika maeneo ya umma ili kuhamamisha wananchi katika matumizi ya teknolojia.
Hayo yamesemwa leo Aprili 11, 2023 na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Janeth Mahawanga aliyehoji serikali haioni haja kufunga mtandao wa Wifi maeneo yote nchini ili jamii ihamasika na matumizi ya teknolojia.
Akijibu swali hilo bungeni jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, Naibu Waziri Kundo Mathew amesema serikali imetekeleza huduma hiyo kwenye vituo sita, ambavyo ni Soko la Tabora, Stendi ya Nanenane Dodoma, Buhongwa Mwanza, Kiembe Samaki Unguja, Chuo Kikuu cha Dodoma kupitia ndaki ya sayansi za komputya na elimu angavu na Chuo cha Ustawi wa Jamii Rungemba.
Naibu waziri huyo amesema kuwa huduma hiyo itaendelea kuwepo maeneo mbalimbali nchini kulingana na upatikanaji wa fedha utakavyokuwa.



