PURA yaandaa ‘mwarobaini’ ukosefu wa vyeti vya usalama miradi ya mafuta, gesi

Mkuu wa Kitengo cha ushirikishwaji wa wazawa na uhusishwaji wa wadau kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Nyangi amebainisha mikakati inayoendelea kutekelezwa ili kutatua kutatua changamoto ya ukosefu vya vyeti vya masuala ya usalama baharini.
Nyangi amelazimika kutoa maelezo hayo baada ya wadau kueleza kuwa ukosefu wa vyeti hivyo unadumaza ushiriki wa Watanzania katika miradi ya utafutaji na uzalishaji wa gesi asilia nchini hususan miradi inayotekelezwa maeneo ya baharini.
Amebainisha hayo wakati akichangia mjadala uliofanyika Zanzibar jana kuhusu changamoto zinazozuia Watanzania kushiriki kikamilifu katika miradi ya mafuta na gesi asilia inayotekelezwa nchini na mikakati ambayo PURA kama Mamlaka inatekeleza kutatua changamoto hizo.
Akizungumzia mkakati wa kutatua moja ya changamoto ya ukosefu wa vyeti vya masuala ya usalama ili kuweza kufanya kazi maeneo ya baharini, Nyangi alieleza kuwa PURA iko mbioni kusaini Makubaliano ya Awali na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (Dar es Salaam Maritime Institute – DMI) kwa lengo la kushirikiana kuanzisha kituo chenye ithibati kinachotambulika duniani kitakachotoa mafunzo hayo nchini.
“Kwa sasa hakuna kituo chenye ithibati nchini Tanzania kinachotoa kozi za masuala ya usalama na tahadhari kama vile Basic Offshore Safety Induction and Emergency Training (BOSIET) yanayowezesha s kupata kibali cha kufanya kazi katika miradi ya mafuta na gesi inayotekelezwa baharini.
Chagamoto hii imepeleka watanzania wenye ujuzi na uwezo wa kufanya kazi katika miradi hiyo kulazimika kwenda nje ya nchi kwa gharama kubwa kusomea kozi hizo.
“Hii ni changamoto kwa kuwa watanzania wachache ndio wanaoweza kumudu gharama za kwenda nje ya nchi kusoma kozi husika,” Nyangi ameongeza.
Kuanzishwa kwa kituo hicho nchini, kwa mujibu wa mkuu huyobwa kitengo, kutawezesha Watanzania wengi zaidi kupata cheti cha usalama na umahiri baharini hivyo kusaidia ongezeko la watanzania wanaoshiriki katika miradi ya mafuta na gesi asilia hususan miradi ya mkondo wa juu wa petroli inayotekelezwa nchini.



