DC: Msikimbilie kuandamana kwa maneno ya uzushi

GEITA; MKUU wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed amewataka wananchi kuwa waangalifu na wasijiingize kwenye mkumbo wa maandamano yanayoweza kusababisha uhalifu wa binadamu na mali zao.
Sakina ametoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari, siku moja baada ya kutokea uhalifu katika Kituo cha Polisi Kata ya Lulembela wilayani humo, kufuatia taarifa za uzushi kuwa kuna wizi wa watoto.

Amesema tukio hilo lilitokea Septemba 11, 2024 siku ya mnada Kata ya Lulembela, ambapo taharuki ilitokana na uzushi wa wananchi kwamba kuna watu wameiba watoto taarifa ambazo hazikuwa na ukweli.
“Hii ilisababisha taharuki kubwa na wananchi kujichukulia sheria mkononi na baadaye wakavamia kituo cha polisi na kufanya uhalifu mkubwa, ikiwemo kuchoma gari lililokuwa maeneo yale,” amesema.
Amewaonya wakazi wa Mbogwe na maeneo ya jirani wasirudie tena kutumia taarifa za uzushi ambazo hazijathibitishwa kufanya maamuzi badala yake hatua za kisheria zifuatwe kuepuka taharuki.
Soma pia: Maandamano Kenya yaua, yajeruhi
“Ni vyema kwa sababu watuhumiwa walikuwa wamefikishwa kituo cha polisi walipaswa wafuate taratibu, wazingatie sheria kama ilivyo utamaduni wetu.
“Niwaombe sana watanzaia wasiendelee kujichukulia sheria mkononi, kwani inasababisha athari kubwa kwa watu wengine wasio wahusika wa tukio hilo,” amesema.
Septemba 11, 2024, msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alithibitisha vijana wawili walifariki dunia baada ya wananchi zaidi ya 800 kuvamia na kufanya vurugu katika kituo cha polisi Lulembela wilayani Mbogwe.



