Wasanii wajitokeza kupima magonjwa ya moyo Dar

DAR ES SALAAM; WASANII mbalimbali wakiongozwa na Mboso Khan na Zuhura Othuman ‘Zuchu’ wamejitokeza kupima magonjwa ya moyo katika kliniki ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Kawe, Dar es Salaam.
Akizungumza na HabariLEO wakati wa upimaji huo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge, amewataja baadhi ya wasanii waliojitokeza kuwa ni Zuchu, Mboso na D voice.
“Niombe wasanii ambao bado hawajajitokeza kupima wajitokeze na wapime ili waishi wakiwa wanazijua afya zao na kuendelea kufanya kazi zao kwa huru zaidi.
“Tulianza na wachezaji mpira na sasa hivi tupo na wasanii ambapo tukimaliza tutatangaza kundi linguine linalofata kuja kupima na kuangalia kama wana matatizo ya moyo.

“Lengo ni kuwasaidia wasanii wasiwe na magonjwa yasioambukiza, lakini pia wawe na kawaida ya kucheki afya zao na kuendelea vizuri na majukumu yao ya kula siku katika kuelimisha na kuburudisha jamii, “amesema Dk Kisenge
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Gervas Kasiga ‘Chuma’ amesema kuwa huduma hiyo ya upimaji itarndelea kuwepo kila jumamosi na Jumapili hadi Januari 2025.
“Tunafurahi kuona wasanii wanaendelea kujitokeza kwa wingi kupama moyo jambo zuri, nitoe wito kwa wengine ambao hawajajitokeza waendelee kujitokeza na kupima kujua afya zao kama wana tatizo hama hawana,” amesema.
Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Kedmon Mapana amesema kuwa: “Rais Samia kwa kushirikiana na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao wameweza kufanikisha hili na wasanii wameanza rasmi kupimwa moyo, niwaombe wajitokeze kwa wingi kupima, “amesema Mapana.



