Yanga yaitangazia vita Al Hilal

DAR ES SALAAM; YANGA imeitangazia vita Al Hilal ya Sudan kwenye mchezo wa raundi ya tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Uwanja Cheikha Ouldi Boidiya, Nouakchott, Mauritania.

Ushindi kwenye mchezo huo utaifanya Yanga kufikisha pointi saba na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuingia hatua ra robo fainali ya michuano hiyo.

Kwenye mchezo wa awali Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Novemba 14, Al Hilal waliifunga Yanga mabao 2-0.

Akizungumza na Crown Fm jana, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe alisema mchezo wao dhidi ya Al Hilal ni vita na mipango yake ni tofauti na mipango ya michezo mingine.

“Hii mechi ina mambo mengi na haihitaji maneno maneno, hii ni vita na mipango yetu ni tofauti na mipango ya mechi nyingine, tunaenda kwenye uwanja wa vita na ramani za vita huwa hazitolewi nje,” alisema Kamwe.

Aidha, alisema kikosi cha timu hiyo kinatarajia kusafiri kesho kuelekea Mauritania kupitia Uturuki kwa ajili ya mchezo huo.

Endapo Yanga itashinda mechi zake mbili zilizosalia dhidi ya Al Hilal Jumapili na ya MC Alger, Uwanja wa Benjamin Mkapa, watafikisha pointi 10 na kuingia hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Habari Zifananazo

Back to top button