Ilani yatekelezwa kwa kishindo Bara, uchumi wapa

UTEKELEZAJI wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwaka 2020-2025 umepandisha kiwango cha ukuaji wa pato la taifa kutoka asilimia 4.8 mwaka 2020 hadi asilimia 5.1 mwaka 2023.
Taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM iliyowasilishwa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ilisema hayo katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa uliomalizika jana jijini Dodoma.
Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kupitia taarifa hiyo alieleza kiwango hicho kilikadiriwa kukua kwa asilimia 5.4 mwaka 2024 na kwamba serikali imedhibiti mfumuko wa bei hadi asilimia 3 mwaka 2024 kutoka asilimia 3.1 mwaka 2020.
“Mapato ya ndani yaliongezeka kufikia Sh trilioni 13.54 mwaka 2024 kutoka Sh trilioni 8.1 mwaka 2020. Idadi ya walipa kodi iliongezeka hadi milioni 6.4, na serikali imeondoa kodi zisizo na tija ili kuchochea maendeleo,” ilieleza taarifa hiyo. Katika kupambana na umaskini na kuwawezesha wananchi kiuchumi, Majaliwa alieleza serikali imeweza kutoa huduma za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kaya 1,357,965 katika vijiji, mitaa na shehia 17,260 Tanzania Bara na Zanzibar.
“Serikali imetekeleza miradi 17,421 ya sekta za afya, elimu na maji na kutoa ajira za muda kwa kaya za walengwa 662,374 Tanzania Bara na Zanzibar, kutoa mikopo isiyo na riba ya Sh bilioni 240.9 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu na kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana 164,443 waliomaliza taasisi za elimu ya juu na kati,” alisema.
Majaliwa alieleza katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola za Marekani bilioni 5.05, zikitosheleza uagizaji wa bidhaa kwa asilimia 4.1. Mauzo ya bidhaa nje ya nchi yaliongezeka kutoka Dola bilioni 8.81 mwaka 2020 hadi Dola bilioni 14.66 mwaka 2024.
“Wastani wa mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka kutoka Sh trilioni 1.47 Novemba, 2020 hadi Sh trilioni 2.37 Novemba, 2024 na Mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) umekua kutoka Sh bilioni 60 mwaka 2020 hadi Sh bilioni 438 mwaka 2024,” alieleza. Vilevile, madeni yaliyohakikiwa ya Sh trilioni 3.47 yamelipwa kwa wakandarasi, watumishi, watoa huduma, wazabuni na madeni mengineyo ya kimkataba na mikopo Sh bilioni 693.9 ilitolewa na serikali kwa wanufaika zaidi ya milioni 1.7 katika sekta za kilimo, mifugo, na uvuvi.



