Wanne wajeruhiwa majibizano polisi na waandamanaji Kenya

KENYA: TAKRIBAN watu wanne wamejeruhiwa kwa risasi baada ya polisi kukabiliana na waandamanaji katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma, iliyoko kaskazini mwa Kenya.
Maelfu ya wakimbizi wanaoishi katika kambi hiyo—ambayo inahifadhi watu waliokimbia vita na ukame kutoka mataifa jirani kama Sudan Kusini, Ethiopia, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo—waliandamana siku ya Jumatatu wakipinga kupunguzwa kwa mgao wa chakula kutokana na changamoto za ufadhili.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), linalosimamia usambazaji wa chakula katika kambi za wakimbizi, lilitangaza mwezi Desemba mwaka jana kuwa mgao wa chakula kwa wakimbizi umepunguzwa hadi asilimia 45 ya kiwango cha chini kinachohitajika kutokana na upungufu wa rasilimali.
SOMA ZAIDI: WFP waikabidhi serikali kituo msaada wa chakula
Kwa miaka kadhaa, WFP imekuwa ikionya kuhusu changamoto za kifedha kutokana na kupungua kwa michango kutoka kwa serikali zinazofadhili shirika hilo.
Siku ya Jumatatu, WFP ilitangaza kufunga ofisi yake nchini Afrika Kusini kufuatia kupunguzwa kwa misaada ya kigeni, hatua iliyoathiriwa na sera za Rais wa Marekani, Donald Trump, za kupunguza misaada ya kimataifa.



